Iran kushiriki kwa ngazi ya juu katika mazishi za Shahidi Nasrallah
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i122868-iran_kushiriki_kwa_ngazi_ya_juu_katika_mazishi_za_shahidi_nasrallah
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Esmaeil Baghaei, amesema Iran itashiriki kwa ngazi ya juu katika mazishi ya aliyekuwa kiongozi wa harakati ya Muqawama ya Hizbullah nchini Lebanon, Sayyed Hassan Nasrallah.
(last modified 2025-02-18T00:54:38+00:00 )
Feb 18, 2025 00:54 UTC
  • Iran kushiriki kwa ngazi ya juu katika mazishi za Shahidi Nasrallah

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Esmaeil Baghaei, amesema Iran itashiriki kwa ngazi ya juu katika mazishi ya aliyekuwa kiongozi wa harakati ya Muqawama ya Hizbullah nchini Lebanon, Sayyed Hassan Nasrallah.

Baghaei aliyasema hayo katika mkutano wake wa kila wiki na waandishi wa habari siku ya Jumatatu.

Jumanne iliyopita, afisa wa Hizbullah alisema kwamba wajumbe kutoka nchi 79 watahudhuria mazishi ya Shahidi Sayyid Hassan Nasrallah na mkuu wa Baraza la Utendaji, Shahidi Sayyid Hashim Safieddine, yaliyopangwa kufanyika tarehe 23 Februari.

Akizungumza na waandishi wa habari, Sheikh Ali Daher, mratibu wa Kamati Kuu ya mazishi ya Mashahidi Nasrallah na Safieddine, alisema kuwa hafla hiyo itakuwa "siku ya kumbukumbu kwa kiongozi wa wanyonge dhidi ya wakandamizaji, na shahidi wa ubinadamu dhidi ya ubeberu."

Nasrallah aliuawa shahidi katika mashambulizi ya anga ya Israel kusini mwa Beirut mnamo Septemba 27, 2024. Kwa kutumia tani 85 za milipuko, ndege za kivita za Israel ziliharibu majengo sita ya makazi katika eneo la Dahiyeh, baada ya kampeni ya wiki nzima ya mabomu iliyolenga maeneo mbalimbali kutoka kusini mwa Lebanon hadi Beirut.

Safieddine naye aliuawa shahidi katika shambulio la Israel mnamo Oktoba 2024.

Hizbullah iliahirisha hafla za mazishi ya viongozi hao wawili kwa sababu ya hofu ya mashambulizi zaidi kutoka Israel wakati wa hafla hizo.