Raia wa Uingereza waliokamatwa Iran  washtakiwa kwa ujasusi
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i122912-raia_wa_uingereza_waliokamatwa_iran_washtakiwa_kwa_ujasusi
Msemaji wa Idara ya Mahakama ya Iran amesema kuwa raia wawili wa Uingereza waliokamatwa hivi karibuni katika mji wa Kerman, kusini mashariki mwa nchi, wameshtakiwa kwa kufanya ujasusi kwa niaba ya mashirika ya kijasusi ya Magharibi.
(last modified 2025-02-18T23:28:15+00:00 )
Feb 18, 2025 23:28 UTC
  • Raia wa Uingereza waliokamatwa Iran  washtakiwa kwa ujasusi

Msemaji wa Idara ya Mahakama ya Iran amesema kuwa raia wawili wa Uingereza waliokamatwa hivi karibuni katika mji wa Kerman, kusini mashariki mwa nchi, wameshtakiwa kwa kufanya ujasusi kwa niaba ya mashirika ya kijasusi ya Magharibi.

Asghar Jahangir amewaambia waandishi wa habari jijini Tehran kwamba, "Watu hawa waliwekwa walifuatiliwa kwa kushirikiana na mashirika ya usalama na walikamatwa na maafisa wa Kitengo cha Kupambana na Majasusi cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu, IRGC, katika Mkoa wa Kerman."

Ameongeza kuwa, kwa kujifanya kuwa wanafanya utafiti, Waingereza hao walikusanya taarifa nyeti katika majimbo kadhaa. Jahangir amesema kuwa wawili hao ambao ni wanandoa, walikamatwa mwezi Januari, ambapo imebainika kuwa walikuwa wakishirikiana na mashirika ya ujasusi ya nchi za Magharibi na mahasimu wengine wa Iran.

Uingereza imewatambua wawili hao kama wanandoa na wametambuliwa kwa majina ya Craig na Lindsay Foreman. Wiki iliyopita, balozi wa Uingereza nchini Iran, Hugo Shorter, alikutana nao katika Ofisi ya Mwendesha Mashtaka wa Umma na Mapinduzi ya Kerman.

Mkutano huo uliandaliwa kwa ombi la balozi wa Uingereza na uliidhinishwa na mamlaka za Idara ya Mahakama za Iran kwa uratibu na vyombo vya usalama.

Iran imekuwa ikiwakamata raia wa kigeni ambao ni majasusi wa madola ajinabi. Nchi za Magharibi mara nyingi zimepinga kukamatwa raia wao, zikidai kuwa waliokamatwa hawana hatia.

Baadhi ya wafungwa hao wameachiliwa kwa misingi ya kibinadamu, huku wengine wakibadilishwana na raia wa Iran walioko kizuizini nje ya nchi.