Rais Pezeshkian: Iran, Qatar zinafungua njia mpya za ushirikiano
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i122942-rais_pezeshkian_iran_qatar_zinafungua_njia_mpya_za_ushirikiano
Rais wa Iran, Masoud Pezeshkian, amesema Tehran na Doha zimefanya maamuzi muhimu ili kuimarisha uhusiano na kufungua njia mpya za ushirikiano.
(last modified 2026-04-19T09:26:01+00:00 )
Feb 19, 2025 12:04 UTC
  • Rais Pezeshkian: Iran, Qatar zinafungua njia mpya za ushirikiano

Rais wa Iran, Masoud Pezeshkian, amesema Tehran na Doha zimefanya maamuzi muhimu ili kuimarisha uhusiano na kufungua njia mpya za ushirikiano.

Akizungumza kwenye mkutano wa waandishi wa habari akiwa na Emir wa Qatar Sheikh Tamim bin Hamad Al Thani baada ya mazungumzo yao mjini Tehran, Pezeshkian amesema wamejadili masuala ya pande mbili ili kulinda maslahi ya mataifa yote mawili.

Rais  wa Iran amesema Emir wa Qatar amesisitiza umuhimu wa kuunda fursa mpya za ushirikiano.

Rais Pezeshkian ameongeza kuwa moja ya sera kuu za Iran ni kukuza uhusiano wa kina na nchi jirani na mataifa ya kanda.

Rais wa Iran aidha amesema pia wamejadili hali ya Syria, ambapo amesisitiza umuhimu wa kuhifadhi umoja wa ardhi na mamlaka ya Syria pamoja na kushirikishwa kwa wananchi wake wote katika kuamua mustakabali wao.

Rais Pezeshkian amepongeza juhudi za upatanishi za Qatar katika kufanikisha usitishaji wa mapigano Gaza na kuachiliwa kwa Wapalestina waliotekwa.

Rais huyo wa Iran amesisitiza haja ya kuchukuliwa hatua thabiti zaidi na mataifa ya Kiislamu ili kupunguza mateso na maumivu ya watu wa Gaza.

Rais Pezeshkian amesema ni muhimu kwa Wapalestina wa Gaza kuishi kwa usalama katika ardhi yao ya kihistoria.

Emir wa Qatar kwa upande wake ameeleza kufurahishwa na ziara yake nchini Iran na ameongeza kuwa ziara kama hizi zinaweza kusaidia kupanua uhusiano wa kihistoria na wa kindugu kati ya mataifa hayo mawili, uhusiano ambao msingi wake mkuu ni ujirani mwema.

Amesema wamejadili ushirikiano katika nyanja mbalimbali na kusisitiza umuhimu wa kuunda fursa zaidi za ushirikiano, hasa katika sekta za biashara na uchumi.

Ujumbe wa Iran ukiongozwa na Rais Masoud Pezeshkian, kulia, katika mkutano na ujumbe wa Qatar unaoongozwa na Emir Sheikh Tamim bin Hamad Al Thani mjini Tehran Februari 19, 2025.

 

Sheikh Tamim anasema pia wamejadili changamoto ngumu zinazokumba eneo la Asia Magharibi.

Emir wa Qatar amesifu sera ya kukuza uhusiano mzuri na mataifa ya Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi pamoja na nchi za Kiislamu kwa misingi ya maslahi ya pamoja na ujirani mwema.

Kuhusu Palestina, Emir wa Qatar amesisitiza umuhimu wa kuheshimu makubaliano ya kusitisha mapigano Gaza na kuhakikisha misaada ya kibinadamu inawafikia watu wa eneo hilo.

Aidha amesema: "Leo, nimemhakikishia Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwamba Qatar na washirika wake wamejitolea kusaidia upatanishi kwa utekelezaji mzuri wa makubaliano haya."

Emir wa Qatar amesema anaamini upatanishi huo ni "hatua muhimu kuelekea usitishaji wa mapigano wa kudumu na endelevu Gaza, pamoja na kuhakikisha misaada ya kibinadamu inawafikia watu bila kizuizi chochote."

Emir wa Qatar ameeleza matumaini kwamba usitishaji wa mapigano utaondoa mateso ya raia wa Gaza, kuweka msingi wa ujenzi upya, na kusaidia kufanikisha suluhisho la haki, endelevu, na jumuishi kwa Palestina.