IRGC ya Iran yavunja mitandao ya ujasusi ya Israel na Marekani
Vikosi vya kiintelijensia vya Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu la Iran (IRGC) vimesambaratisha mitandao kadhaa ya kijasusi yenye mfungamano na Marekani na Israel katika mkoa wa Mazandaran, kaskazini mwa nchi.
Brigedia Jenerali Siavash Moslemi, Kamanda wa IRGC katika mkoa huo alitangaza habari ya operesheni hiyo katika taarifa ya jana Jumatano akisema kwamba, operesheni hiyo sio tu ilizima vitisho vikubwa vya usalama, lakini pia ilizuia migororo ambayo ingeweza kutokea hapa nchini.
Ameeleza kuwa, idara za kijasusi kutoka Israel, Marekani, na nchi nyingine zenye uhasama zimekuwa zikijaribu kujipenyeza nchini Iran, huku majasusi wao wakijifanya raia wa kigeni na watu waliokimbia makazi yao.
Brigedia Jenerali Moslemi amesema wengi wa maajenti hao walikuwa wakifanya kazi chini ya kivuli cha makampuni ya kibiashara, vituo vya kitamaduni, na mashirika ya kutoa misaada, huku wakiwa lengo la kukusanya data hasisi, au kuanzisha mitandao ya ushawishi ndani ya Iran.
Kamanda huyo wa IRGC katika mkoa wa Mazandaran amebainisha kwamba, vikosi vya SEPAH vimefaulu kubaini na kusambaratisha mitandao hiyo ya ujasusi ya maadui kutokana na ufuatiliaji sahihi wa vikosi vya kiintelijensia vya Iran.
Huko nyuma pia, vikosi vya Wizara ya Intelijensia ya Iran vilifanikiwa kusambaratisha mtandao wa magaidi wa Shirika la Kijasusi la Utawala wa Kizayuni wa Israel (Mossad) magharibi mwa nchi.