Araghchi: Iran haitafanya mazungumzo na Marekani maadamu mashinikizo yapo
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi, katika mkutano wa pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia, Sergey Lavrov, mjini Tehran, amesea hakuna mazungumzo ya moja kwa moja kati ya Iran na Marekani yatakayofanyika maadamu Washington inaendeleza sera sera 'Mashinikizo ya Juu Zaidi' dhidi ya Iran.
Araghchi, amefafanua kuwa Iran inaendelea na mashauriano ya karibu na Russia kuhusu mipango ya nyuklia, akisisitiza kuwa Iran iko tayari kushirikiana na washirika wake kama China na Russia kuhusu msimamo wake.
Ameongeza kuwa mazungumzo hayo hayahusu tu masuala ya pande mbili, bali pia yanagusia masuala makubwa ya kikanda, ikiwa ni pamoja na Palestina, Lebanon, Syria, na mpango wa hivi karibuni wa Rais wa Marekani wa kuhamisha kwa nguvu Wapalestina wa Gaza. Iran imelaani vikali mpango huo wa Trump.
Kwa upande wake Lavrov amesema bado kuna nafasi ya diplomasia katika kutafuta suluhisho linalokubalika kwa pande zote kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran.
"Tumezungumza kwa kina kuhusu hali inayohusiana na Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA) kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran," alibainisha. "Tunaamini kuwa rasilimali za kidiplomasia bado hazijatumika kikamilifu na hazipaswi kupuuzwa. Zinapaswa kutumiwa kwa ufanisi, bila vitisho au dalili za suluhisho la kijeshi."
Mwanadiplomasia huyo wa ngazi za juu wa Russia amesisitiza kuwa pande zote mbili zinaendelea kujitolea "kuendeleza juhudi za kutafuta suluhisho linalokubalika kwa pande zote ili kutoka kwenye hali ya sasa," ambayo, alisisitiza, ilisababishwa na mataifa ya Magharibi na si Iran.
Iran na Russia ni mataifa mawili yenye uhusiano wa karibu nahivi karibuni yamepanua ushirikiano wao katika sekta za kijeshi na kiuchumi. Kutokana na vikwazo vya Marekani, ushirikiano wao ndani ya BRICS na Shirika la Ushirikiano la Shanghai, hasa kwa ajili ya kupunguza mivutano, unaweza kusaidia kukuza uchumi wa mataifa yote mawili.