IRGC yasisitiza: Operesheni ya Ahadi ya Kweli 3 itatekelezwa kwa wakati uliopangwa
Kamanda mwandamizi wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu IRGC ametangaza kuwa, awamu ya tatu ya Operesheni ya "Ahadi ya Kweli" itatekelezwa katika wakati uliopangwa, kufuatia utekelezaji uliofanikiwa wa awamu yake ya kwanza na ya pili.
Ali Fazli, Naibu Mratibu wa IRGC, amethibitisha kutekelezwa kwa operesheni hiyo, akisisitiza umuhimu wake wa kimkakati. "Awamu ya kwanza na ya pili ya "Ahadi ya Kweli" tayari imekamilika, na awamu ya tatu itaendelea kama ilivyopangwa," amesema kamanda huyo.
Amesema kama ambavyo awamu ya kwanza na ya pili ya operesheni hiyo zilifanikiwa kikamilifu, Operesheni ya "Ahadi ya Kweli" ya Tatu itapata mafanikio na itatekelezwa kwa wakati ulioanishwa.
Kadhalika mwezi uliopita, Kamanda wa ngazi za juu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) alisema, Iran "lazima iwe tayari kwa vita, ili kusiwepo na vita".
Brigedia Jenerali Amir Ali Hajizadeh, Kamanda wa Kikosi cha Anga za Mbali cha IRGC, alieleza hayo katika mahojiano na televisheni ya hapa nchini. Alisema operesheni ya tatu ya kulipiza kisasi dhidi ya utawala wa Kizayuni wa Israel itatekelezwa.
Aidha Disemba 2024, Naibu Kamanda wa IRGC Admeli Ali Fadavi aliapa kwamba operesheni ya tatu ya Ahadi ya Kweli itatekelezwa kujibu shambulio la anga la Israel la Oktoba 26,2024, ambalo liliua shahidi Wairani wanne.