Kuwa tayari Iran kuimarisha uhusiano na nchi za Kiafrika
(last modified Sun, 02 Mar 2025 02:33:25 GMT )
Mar 02, 2025 02:33 UTC
  • Kuwa tayari Iran kuimarisha uhusiano na nchi za Kiafrika

Mshauri na Mjumbe Maalumu wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amekutana na kuzungumza na Waziri wa Mambo ya Nje wa Ethiopia na kusisitiza kuwa Iran iko tayari kuimarisha uhusiano na Ethiopia na nchi za Kiafrika kwa ujumla.

Is'haq Al Habib ambaye yuko ziarani mjini Addis Ababa kwa ajili ya mazungumzo na viongozi wa Ethiopia, amekutana na kuzungumza na Gideon Timothy, Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo. 

Pande mbili zimeashiria uhusiano wa muda mrefu kati ya Iran na Ethiopia na kubadilishana mawazo kuhusu njia za ustawi na kuboresha uhusiano na ushirikiano kati ya nchi mbili katika nyanja mbalimbali na pia katika taasisi za kikanda na kimataifa. 

Mbali na nyanja za kiuchumi na kibiashara, katika miaka ya karibuni Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekuwa ikitoa kipaumbele na kutilia maanani uhusiano wa kisiasa kati yake na nchi za bara la Afrika. Nchi 50 kati ya 54 za bara hilo ni wanachama wa Jumuiya ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote (NAM), na baadhi ya nchi hizo zimewekewa vikwazo. Aidha kuna nchi 30 za Kiislamu katika bara la Afrika na karibu asilimia 50 ya watu wake ni Waislamu; jambo ambalo lina umuhimu pia kwa Iran kwa upande wa kiutamaduni. 

Viongozi wa Jumuiya ya NAM 

Mbali na kuwa na utajiri wa rasilimali, bara la Afrika linaweza kuwa mshirika bora wa Iran kwa upande wa kiuchumi na wakati huo huo Afrika inaweza kuwa na mchango katika kuiunga mkono Iran katika taasisi za kikanda na kimataifa katika upande wa kisiasa. jambo hilo muhimu linaweza kutimia kupitia masuala yanayozikutanisha pamoja pande hizo mbili, yaani Iran na Afrika. 

Irada na azma ya viongozi wa Iran na nchi za Kiafrika ni kuistawisha uhusiano kadiri inavyowezekana, na kuna fursa nyingi katika nyanja za teknolojia, mawasiliano, maeneo ya viwanda, mitambo ya kuzalisha umeme, nishati mpya, ujenzi wa nyumba, vifaa tiba na kilimo, ambazo zinaweza kujumuishwa katika ajenda ya utekelezaji ya maafisa wa pande mbili, na pia  kuanzisha safari za mara kwa mara za meli, ujenzi wa miundombinu, na kusaini makubaliano ya kupunguza ushuru wa kibiashara kati ya Iran na Afrika.

Nchi za Kiafrika zinaunda theluthi moja ya nchi za dunia nzima; kwa msingi huo kuimarisha uhusiano na nchi hizo kunaweza kupanua wigo wa kuungwa mkono Iran kimataifa, nchi ambayo inakabiliwa na vikwazo haramu vya Magharibi na Marekani.

Kwa mtazamo wa kisiasa pia, suala la kustawisha uhusiano na nchi za bara la Afrika ni muhimu kwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. 

Kuwekeza vitega uchumi na kushiriki pakubwa Iran barani Afrika si tu ni kwa ajili ya manufaa ya kiuchumi ya pande mbili bali pia kutazidisha hadhi na ushawishi wa kisiasa na kiutamaduni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika bara hilo. Kwa mantiki hiyo, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran hasa katika miaka ya hivi karibuni, imeupa umuhimu uhusiano wa kidiplomasia na kuitisha vikao vya pande mbili na nchi mbalimbali za Afrika.

Katika miaka ya hivi karibuni, Iran imepanua uhusiano wake na nchi wanachama wa Umoja wa Afrika (AU) katika nyanja mbalimbali za kiuchumi, kisiasa na kiutamaduni na imechaguliwa kuwa mwanachama mtazamaji wa umoja huo. 

Wakuu wa Kiafrika katika Mkutano wa 38 mjini Addis Ababa

Iran ina uwezo na suhula mbalimbali kwa ajili ya kupanua uhusiano na nchi za Kiafrika na nyanja za pamoja za kisiasa na kiuchumi zinaandaa mazingira ya kuimarisha uhusiano huo. Malengo muhimu zaidi ya Iran ya kustawisha uhusiano na nchi za Kiafrika ni kwa ajili ya kushirikiana kiuchumi kwa kunufaika na teknolojia mpya na kuwekeza katika bara hilo ambalo nchi zake ni jukwaa linalofaa na lenye uwezo kwa ajili ya ushirikiano.