Spika: Mataifa yanayotegemea usalama kutoka nje yatafeli
(last modified Sun, 02 Mar 2025 12:26:55 GMT )
Mar 02, 2025 12:26 UTC
  • Spika: Mataifa yanayotegemea usalama kutoka nje yatafeli

Mohammad Baqer Qalibaf, Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) amesema mustakabali wa nchi zinazotegemea mataifa mengine kwa ajili ya kudhaminiwa usalama na maendeleo ni kufeli na kugonga mwamba.

Qalibaf amesema hayo katika kikao cha wazi cha Bunge hapa mjini Tehran leo Jumapili na kutangaza bayana kwamba, "Kutegemea nguvu za nje, haswa mabeberu, kutasababisha kushindwa kusikoweza kuepukika."

"Leo hii, dhati na taswira halisi ya madhalimu imefichuliwa duniani," Spika wa Bunge la Iran amesema, bila kuashiria moja kwa moja tukio la karibuni la Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky kudhalilishwa na Rais Donald Trump wa Marekani katika Ikulu ya White House.

Katika mkutano huo wa Ijumaa uliotibuka baada ya vita vya maneno, Trump alimshutumu Zelensky kwa kutoonyesha shukrani za kutosha kwa msaada wa kijeshi na kifedha wa Marekani kwa Kiev.

Akielezea Mapinduzi ya Kiislamu kuwa ni Mapambano ya Kimantiki yaliyolikomboa taifa la Iran kutoka katika utegemezi wa madola yasiyoaminika, Spika Qalibaf amesema kuwa madola hayo ya kiistikbari yanawanyonya washirika wao kwa ahadi za uwongo, ili kuendeleza malengo yao maovu, na kisha kuyatupilia mbali baadaye.

Spika wa Majlsi ya Ushauri ya Kiislamu ameongeza kuwa, ingawa kuwapinga wakandamizaji kunaweza kuwa kugumu au kwa gharama kubwa, kuegemea upande wao na kuungana nao hatimaye huwa na matokeo mabaya hata zaidi.