Spika Qalibaf: Snapback ni batili, Iran itajibu mapigo
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i131352-spika_qalibaf_snapback_ni_batili_iran_itajibu_mapigo
Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran), Mohammad-Baqer Qalibaf amepinga uamilishaji wa utaratibu wa snapback wa kurejeshewa Iran vikwazo, na kuitaja hatua hiyo kuwa ni kinyume cha sheria; huku akisisitiza kuwa Jamhuri ya Kiislamu haina wajibu wa kuheshimu uamuzi huo ulioshinikizwa na Troika ya Ulaya.
(last modified 2025-09-28T11:45:10+00:00 )
Sep 28, 2025 11:45 UTC
  • Spika Qalibaf: Snapback ni batili, Iran itajibu mapigo

Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran), Mohammad-Baqer Qalibaf amepinga uamilishaji wa utaratibu wa snapback wa kurejeshewa Iran vikwazo, na kuitaja hatua hiyo kuwa ni kinyume cha sheria; huku akisisitiza kuwa Jamhuri ya Kiislamu haina wajibu wa kuheshimu uamuzi huo ulioshinikizwa na Troika ya Ulaya.

Qalibaf amebainisha kuwa, Russia na China, zikiwa wanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, pia zimesisitiza uharamu wa kuamilishwa utaratibu huo.

Spika wa Bunge la Iran amesema vikwazo vilivyopendekezwa katika azimio hilo vina uzito mdogo ikilinganishwa na vikwazo vya Marekani. "Hata hivyo, ikiwa nchi yoyote itachukua hatua dhidi ya Iran kwa kuzingatia maazimio haya haramu, itakabiliwa na jibu madhubuti kutoka kwa Iran," Qalibaf ameonya.

Akirejelea juhudi za kidiplomasia za Iran kusuluhisha suala hilo, ikiwa ni pamoja na Mkataba wa Cairo, Qalibaf amesema kuwa nchi za Magharibi zinatumia mazungumzo kama chombo cha kuhadaa na kuishinikiza Iran ili iachane na mpango wake wa makombora.

"Kwa Iran, diplomasia daima imekuwa njia ya kutetea haki zake na itasalia kuwa hivyo. Lakini imedhihirika kuwa diplomasia bila misingi imara hutumika kama chombo cha mashinikizo," ameongeza.

Akizungumzia vitisho vya Israel, Spika wa Bunge la Iran amesema: "Ikiwa Israel haijaishambulia Iran hadi sasa, si kwa sababu mfumo wa snapback ulikuwa haujaamilishwa, lakini kwa sababu inajua shambulio jingine lingeleta ushindi mkubwa zaidi kuliko vita vya awali (vya siku 12)."

"Njia pekee ya kuwazuia maadui kuishambulia Iran ni kuimarisha vipengele vya mamlaka na kudumisha umoja wa kitaifa," Qalibaf amesisitiza.