Ghalibaf: Hizbullah ipo hai na inaendelea na harakati zake
Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran), Mohammad Bagher Ghalibaf amesisitiza kuwa Harakati ya Muqawama ya Hizbullah ya Lebanon ingali "hai na inafanya kazi zake kama kawaida", huku ikiungwa mkono na wananchi wa nchi hiyo ya Kiarabu.
Ghalibaf aliyasema hayo katika hafla iliyofanyika kuadhimisha mwaka mmoja tangu kuuawa shahidi Sayyid Hassan Nasrullah na Sayyid Hashem Safieddine, Makatibu Wakuu wa zamani wa Hizbullah, katika mkoa wa Qom katikati mwa Iran.
Amesema Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na wananchi wake wameonyesha kupitia kusimama kidete, mshikamano na uungaji mkono wao usioyumba kwa upande wa muqawama na Hizbullah kwamba hawatasalimu amri mbele ya vitendo vya uchokozi na kusisitiza kwamba kupitia umoja wa kitaifa na ushirikishwaji wa umma, watadumisha na kuimarisha uwezo na nguvu ya muqawama.
Spika Ghalibaf ameongeza kuwa, utawala ghasibu wa Israel umeonyesha rekodi ya ukaliaji mabavu, uchokozi na ukiukaji wa haki za mataifa kwa muda wa miaka 77 iliyopita.
"Hata wakati ambapo utawala wa [Israel] ulionekana kutangaza amani au kusitisha mapigano, umekuwa ukijaribu kulazimisha vita na kutawala nchi katika eneo hilo. Historia ya vitendo vyake inafichua dhati yake ya uadui na mwelekeo wa vurugu dhidi ya raia," Ghalibaf amesisitiza.
Akirejelea mienendo ya kihistoria ya utawala ghasibu wa Israel, amesema kuwa asili ya utawala huo imekuwa na sifa ya kulazimisha vita badala ya amani. "Uzoefu kutoka Camp David, Oslo, na Oslo II unaonyesha kwamba utawala huu haukuonyesha huruma hata kwa wale waliojadiliana nao," ameongeza.
Hivi karibuni, wafuasi wa Hizbullah na makundi mengine ya Muqawama ya nchi hiyo walifanya maandamano makubwa katika mji mkuu Beirut, wakipinga vikali pendekezo la baraza la mawaziri linaloungwa mkono na Marekani na Israel la kuwapokonya silaha wanamuqawama.