Pezeshkian: Ramadhani iwe chachu ya kuimarika umoja wa Waislamu
(last modified Mon, 03 Mar 2025 07:08:10 GMT )
Mar 03, 2025 07:08 UTC
  • Pezeshkian: Ramadhani iwe chachu ya kuimarika umoja wa Waislamu

Rais Masoud Pezeshkian wa Iran sambamba na kuwapongeza viongozi na mataifa ya Kiislamu kwa mnasaba wa kuwadia mwezi mtukufu wa Ramadhani, ametoa mwito kwa nchi za Kiislamu kuutumia mwezi huu wa baraka kama chachu ya kuimarisha umoja, mshikamano na ushirikiano miongoni mwao.

Katika ujumbe wake siku ya Jumapili, Pezeshkian amesema anatumai Ramadhani hii itatumika kama kichocheo cha kuimarisha uhusiano na ushirikiano miongoni mwa mataifa ya dunia.

"Kwa baraka za mwezi huu, tunatarajia kupanuka kwa ushirikiano miongoni mwa nchi za Kiislamu," imesema sehemu moja ya ujumbe huo wa Pezeshkian.

Ameitaja Ramadhani, ambayo inatofautishwa na miezi mingine kwa fadhila zake kubwa na nyingi, kama fursa adhimu ya kutafakari zaidi na kutadaburi juu ya uumbaji wa binadamu na ulimwengu, pamoja na kutimiza amri za Mwenyezi Mungu za ukarimu na wema.

Kadhalika ujumbe huo wa Ramadhani wa Rais wa Iran umeangazia masaibu ya watu wa Palestina na Lebanon.

Wapalestina wakifuturu pamoja kando ya vifusi

Amesema, "Kwa baraka za mwezi huu na kupitia juhudi za pamoja za viongozi wa nchi za Kiislamu, tunatumai kupunguza mateso ya taifa la Palestina na haswa watu wa Gaza na Lebanon."

Rais wa Iran amesisitiza umuhimu wa kustawisha umoja kati ya nchi za Kiislamu na kusisitiza kuwa utawala wa Kizayuni unafanya jinai kwa sababu ya mifarakano miongoni mwa Waislamu.

Rais Pezeshkian amesisitiza kuwa, kuimarisha maelewano na uhusiano miongoni mwa nchi za Kiislamu ni miongoni mwa mambo ya lazima katika hali ya sasa ya dunia.