Iran yakemea mauaji ya waliowachache nchini Syria, yataka yakomeshwe
Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imetoa tamko kali la kulaani mauaji ya raia nchini Syria, ikielezea machafuko hayo kuwa ni umwagaji damu usiokubalika pamoja na vitendo vyovyote vya uhasama vinavyolenga makundi ya wachache katika nchi hiyo ya Kiarabu.
Msemaji wa wizara hiyo, Esmaeil Baghaei, amesema katika mkutano na waandishi wa habari siku ya Jumatatu kwamba,"Katika siku za hivi karibuni, matukio ya kusikitisha yamefanyika katika maeneo fulani ya Syria. Tunahofia sana ripoti za ukosefu wa usalama na ghasia."
Ameongeza kuwa:“Tunalaani vikali vitendo hivyo, na mauaji yoyote ya halaiki au mashambulizi dhidi ya raia hayakubaliki na hayana uhalali wowote.”
Kauli hiyo imetolewa wakati ripoti zinaendelea kuonyesha kuongezeka kwa machafuko kaskazini-magharibi mwa Syria, ambapo familia nzima zimeripotiwa kuuawa katika mapigano yanayozidi kupamba moto.
Idadi ya waliouawa kutokana na ghasia hizo imepanda na kufikia zaidi ya watu 1,000 ndani ya siku mbili pekee, wakiwemo raia 745 waliouawa kikatili kwa njia ya kunyongwa au kupigwa risasi kwa njia ya utekelezaji wa hukumu.
Pia, wapiganaji 125 wa kundi linaloongozwa na Hay'at Tahrir al-Sham (HTS) pamoja na karibu wanachama 150 wa makundi ya upinzani wameripotiwa kuuawa, kwa mujibu wa shirika la uangalizi la Syrian Observatory for Human Rights, lenye makazi nchini Uingereza.
Mapigano hayo yalizuka katika eneo la pwani kaskazini-magharibi mwa Syria siku ya Alhamisi, eneo ambalo linakaliwa zaidi na watu wa madhehebu ya Alawi.
Baghaei amesisitiza kuwa "ukweli kwamba jamii fulani za Waalawi zinalengwa, umeumiza dhamiri za watu kote duniani." Amelitaja tukio hilo kuwa ni "jaribio halisi" kwa utawala unaoongozwa na Hay'at Tahrir al-Sham katika kutimiza wajibu wake wa "kulinda maisha ya Wasyria."
Aidha amesema: “Tumewasilisha wasiwasi wetu kupitia njia zinazofaa kwa mataifa yenye ushawishi mkubwa. Matukio kama haya yanazidi kuifanya hali ya kisiasa ya Syria kuwa ngumu zaidi."