Balozi: Mkutano wa Baraza la Usalama la UN Kuhusu Iran ni ‘Mbinu Mbaya ya Kisiasa'
Balozi wa Iran katika Umoja wa Mataifa amelaani mkutano wa Baraza la Usalama kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran, akiuita "mbinu mbaya ya kisiasa " inayotumiwa vibaya na chombo hicho cha kimataifa ili "kutimiza ajenda finyu".
Katika taarifa yake Alhamisi, Amir Saeid Iravani amesema mkutano huo ni "uingiliaji wa kiholela" katika ushirikiano unaoendelea kati ya Iran na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA).
Amesema: "Tunapinga vikali mkutano huu wa kichochezi na usio wa lazima. Huu si mijadala halali kuhusu kuzuia uenezaji wa silaha za nyuklia—bali ni mbinu ya kisiasa inayotumiwa vibaya na Baraza la Usalama kutimiza malengo binafsi."
Aidha amesema: "Vitendo kama hivi vinaweka mfano mbaya unaodhoofisha uaminifu wa Baraza la Usalama."
Mkutano huo wa faragha kuhusu mpango wa nyuklia wa Tehran uliitishwa na Uingereza, Ufaransa na Ujerumani kwa ombi la Washington, siku chache baada ya Bodi ya Magavana ya IAEA kutoa maoni yake kuhusu suala hilo.
Balozi Iravani amesema: "Tunakataa kabisa madai yasiyo na msingi yaliyotolewa na Marekani, Uingereza na Ufaransa. Nchi hizi zimepuuza ukweli kwamba wao wenyewe ndio waliochangia hali ya sasa."
Aidha amesema lengo pekee la mkutano huo ni "kuendeleza sera iliyoshindwa na isiyo halali ya shinikizo la juu dhidi ya Iran," akimaanisha sera ya Rais wa Marekani, Donald Trump, ya kuiwekea Iran vikwazo vikali tangu alipoingia madarakani.
Amesisitiza kuwa ni Marekani iliyojitoa katika makubaliano ya nyuklia ya JCPO mnamo mwaka 2018, ikivunja moja kwa moja Azimio la Baraza la Usalama Na. 2231, na kisha ikaweka upya vikwazo haramu dhidi ya Iran, jambo ambalo liliathiri vibaya wananchi wa Iran.
Mwanadiplomasia huyo wa Iran ameongeza kuwa: "Na ni Uingereza, Ufaransa, na Ujerumani—nchi za Ulaya ndani ya makubaliano ya JCPOA—ambazo, badala ya kutekeleza ahadi zao, zilichagua kuiridhisha Washington kwa kushindwa kutimiza majukumu yao."
Amesisitiza kuwa: "Baraza la Usalama halipaswi kutumiwa na wale wanaopuuza maazimio yake wenyewe huku wakiwashinikiza wengine kuyaheshimu."