Araqchi: Iran iko tayari kuzungumza na Ulaya katika mazingira ya kuheshimiana
(last modified Sun, 16 Mar 2025 02:50:08 GMT )
Mar 16, 2025 02:50 UTC
  • Araqchi: Iran iko tayari kuzungumza na Ulaya katika mazingira ya kuheshimiana

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema: Tehran iko tayari kuzungumza na nchi za Ulaya katika mazingira ya kuheshimiana na yanayojali maslahi ya pamoja.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Sayyid Abbas Araqchi ameyasema hayo katika mazungumzo yake ya simu na mwenzake wa Uholanzi, Caspar Veldkamp ambapo pande hizo mbili zimebadilishana mawazo kuhusu masuala ya uhusiano wa pande mbili na matukio ya kikanda na kimataifa.

Sayyid Abbas Araqchi amesisitiza sera ya Serikali ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ya kuendeleza uhusiano mzuri wa kidiplomasia na nchi nyingine, na kusema Iran iko tayari kwa ajili ya mazungumzo katika mazingira ya kuheshimiana.

Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Uholanzi ameashiria historia ndefu ya uhusiano wa nchi hiyo na Iran na umuhimu wa mchango na nafasi ya Iran katika maendeleo ya kieneo, na kusisitiza udharura wa kutumiwa uwezo wote wa kidiplomasia kwa ajilii ya kujenga maelewano katika mahusiano baina ya nchi na kutatua tofauti zilizopo.

Matamshi ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran yametolewa siku kadhaa tu baada ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kukataa mazungumzo yoyote ya kulazimishwa na kusisitiza kuwa haitafanya mazungumzo kwa shinikizo na vitisho.

Awali, Sayyid Abbas Araqchi, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran aliandika katika ujumbe wake akijibu matamshi ya vitisho ya Trump kuhusu kuilazimisha Iran kufanya mazungumzo kwamba: "Mazungumzo ni tofauti na utumiaji wa mabavu na kushurutisha. Hatutafanya mazungumzo chini ya mashinikizo na vitisho. Mazungumzo kama hayo hayafai hata kujadiliwa, haijalishi ni mada gani (ya kujadiliwa)."