Umuhimu wa kuimarishwa uhusiano wa Iran na India katika nyanja mbalimbali
Seyyed Abbas Araghchi, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameandika katika akaunti yake ya mtandao wa kijamii wa X akiashiria historia ndefu ya uhusiano kati ya nchi mbili za Iran na India kwamba: Uhusiano huu umekuwa muhimu sana katika kuandaa mazingira ya kuimarishwa ushirikiano wa pande zote.
Ameendelea kusema: Leo tunaadhimisha mwaka wa 75 wa kuanzishwa uhusiano kati ya serikali za kisasa za Iran na India.
Akirejelea historia ndefu ya uhusiano kati ya nchi hizi, Araghchi amesema: Bila shaka, historia yetu ya pamoja na uhusiano wa kitamaduni unarudi nyuma kwa karne, kama sio milenia, kwa njia ambayo imeunganisha mataifa haya mawili kwa njia isiyoweza kutenganishwa.
Subramanyam Jaishankar, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa India, akijibu ujumbe wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran kwa mnasaba wa kuadhimishwa miaka 75 ya uhusiano wa Iran na India, ameandika katika akaunti yake ya X kwamba: "Mahusiano ya kina kati ya Tehran na New Delhi yanatokana na uhusiano wa kihistoria. Nina imani kuwa ushirikiano wetu utaendelea kupanuka katika siku zijazo."
Uhusiano kati ya Iran na India una taathira kwa nchi mbili na eneo zima katika masuala ya kiuchumi, kisiasa, kiutamaduni na kiusalama.
India daima imekuwa mojawapo ya washirika wakubwa wa biashara wa Iran katika miaka ya hivi karibuni. Nchi zote mbili zinataka kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara. Iran ina jukumu muhimu katika sekta ya nishati kama muuzaji wa rasilimali za nishati kwa India, haswa mafuta na gesi. Kwa upande mwingine, India pia inashirikiana na Iran katika nyanja mbalimbali kama vile teknolojia ya habari, dawa, viwanda na sekta nyingine.

Kwa kuzingatia nafasi ya kistratijia ya Iran na umuhimu wa bandari za kusini mwa nchi, viongozi wa India siku zote wamekuwa wakitaka kuongeza mabadilishano ya kibiashara ya nchi hiyo na Iran kupitia bahari, jambo ambalo lina umuhimu mkubwa wa kiuchumi kwa India. Hivyo, serikali ya India imeshiriki katika mradi wa kuendeleza bandari ya Chabahar katika mkoa wa Sistan na Baluchistan kusini mashariki mwa Iran. Bandari ya Chabahar nchini Iran inajulikana kama ukanda muhimu wa usafiri wa India, ambao hurahisisha ufikiaji wa India katika nchi za Afghanistan, Asia ya Kati na hata Russia.
Uhusiano wa karibu na Iran ni muhimu sana kwa serikali ya India kwa sababu nchi hii inahitaji ushirikiano na Iran katika kuleta usawa wa kieneo na kulinda maslahi yake ya muda mrefu ya usalama na kiuchumi katika eneo, ikiwa ni pamoja na nchini Afghanistan; makubaliano ya pande tatu kati ya Iran, India na Afghanistan kwenye ukanda unaopangwa kufika Afghanistan na Asia ya Kati kutokea Chabahar, pamoja na ukanda wa kimataifa wa usafirishaji wa Kaskazini-Kusini. Hayo ni miongoni mwa mambo muhimu yanayoifanya India iitazame Iran kwa jicho la kimkakati.
Iran na India pia zinashirikiana katika uga wa masuala ya usalama na mapambano dhidi ya ugaidi. Ushirikiano huu ni muhimu sana katika uwanja wa usalama wa kikanda, ikiwemo Afghanistan, na juhudi za kukabiliana na vitisho vya pamoja.
Iran na India zina uhusiano wa kina wa kitamaduni na kihistoria. Mahusiano ya kitamaduni kati ya nchi mbili hizi yanarudi nyuma hadi kwenye karne zilizopita ambapo uhusiano huu unaendelea kuimarika kupitia lugha na fasihi.
Iran na India sio tu zina uwezo unaohitajika wa kushawishi maendeleo ya kikanda na kimataifa ndani ya mfumo wa mashirika ya kikanda kama vile BRICS na Jumuiya Isiyofungamana na Siasa za Upande Wowote NAM; bali pia kutokana na mambo mengi yanayofanana katika masuala ya kikanda na kimataifa. Tehran na New Delhi zinaweza kuathiri masuala ya kikanda na kimataifa kwa kushauriana zaidi na kuchukua hatua za pamoja.
Ujumbe wa Araghchi na majibu ya Waziri wa Mambo ya Nje wa India yanaonyesha kuwa, Iran na India zinakusudia kupanua zaidi ushirikiano wao wa kisiasa, kiuchumi na kiutamaduni, na ili kufikia lengo hilo, uwezo wa nchi hizi utakuwa na nafasi kubwa katika kustawisha uhusiano. Ushirikiano wa pande mbili kati ya Iran na India katika sekta ya siasa, uchumi na usalama pia utakuwa na nafasi muhimu katika kuboresha hali ya eneo na bara zima la Asia.