Gharibabadi: Iran haina haja ya kupoteza muda kwenye mazungumzo
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje anayehusika na Sheria na Masuala ya Kimataifa amesema kuwa duru ijayo ya mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja kati ya Iran na Marekani itafanyika kama ilivyopangwa na kwamba Tehran haina haja ya kupoteza muda.
Kazem Gharibabadi amesema hayo kwenye mahojiano maalumu na kuongeza kuwa, Iran daima imekuwa ikiingia kwenye mazungumzo kwa umakini na imekuwa mkweli na makini pia katika kutekeleza ahadi zake. Amesema: Kwenye duru ya kwanza ya mazungumzo hayo, Iran ilitangaza wazi kwamba, haitaki kupoteza muda.
Amesema: Mradi wa nyuklia wa Iran ni wa amani kikamilifu. Hakuna chochote cha kusababisha kuwe na wasiwasi na imethibitishwa kiutalaamu kuwa shughuli za nyuklia za Iran hazijaelekea kabisa upande wa kijeshi.
Aidha amesema: Tumewekewa vikwazo vya kikatili na haramu, hivyo lazima viondolewe kwa njia ambayo itawanufaisha watu wetu kivitendo na sio kwenye karatasi tu.
Kwa mara nyingine tena, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ametilia mkazo msimamo wa Tehran wa kwamba hakuna maudhui nyingine yoyote ya kujadiliwa kwenye mazungumzo hayo isipokuwa mradi wa nyuklia na kuondolewa vikwazo.
Gharibabadi ameongeza kuwa: "Katika awamu ya kwanza ya mazungumzo hayo yaliyofanyika mjini Muscat, pande zote mbili zilijiandaa kuendelea na mazungumzo kwa siku ya pili kama ingelazimu, lakini tuliona kwamba masuala yote muhimu yalijadiliwa chini ya saa tatu na lengo lilifikiwa."
Amesema: suala la kurutubisha urani si kitu kinachoweza kuwekwa mezani na kujadiliwa katika mazungumzo hayo.
Amma kuhusu kauli zinazokinzana za Steve Witkoff, mkuu wa timu ya mazungumzo ya Marekani, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema: "Kwa kawaida, kilicho muhimu kwa mkuu wa timu ya mazungumzo ni kufahamu maoni na misimamo ya upande wa pili kwenye meza ya mazungumzo hayo. Bila ya shaka, hatuwezi kupuuza misimamo ya vyombo vya habari vya upande unaopingana nasi katika uchanganuzi wetu. Lazima tuzingatie kila nafasi."