Araghchi: China na Russia ni washirika wa kimkakati wa Iran
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema mara baada ya kuwasili nchini China kwamba, madhumuni ya ziara hiyo ni kuwasilisha ujumbe wa Rais wa Iran kwa maafisa wa China.
Sayyid Abbas Araghchi amebainisha kwamba, China na Russia ni washirika wetu wawili wa kimkakati na marafiki wa karibu, na wamesimama nasi wakati wa matatizo, na siku zote tumekuwa na mashauriano ya mara kwa mara na China katika nyanja mbalimbali.
Akiashiria kuwa safari hii inafanyika sambamba na kukaribia duru ijayo ya mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja kati ya Iran na Marekani, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema: "Katika safari hii, tunakusudia kuwafahamisha kikamilifu marafiki zetu walioko China kuhusu mchakato wa mazungumzo hayo."
Araqchi amesema: China siku zote imekuwa na nafasi ya kujenga mambo katika masuala ya nyuklia ya Iran na itaendelea kufanya hivyo.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema: "China ikiwa mmoja wa wanachama wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na mjumbe wa Bodi ya Magavana wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki, na mshirika wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, daima imekuwa ikishirikiana na Iran katika uga wa nyuklia, na tutaendelea na mashauriano yetu na Beijing."
Araghchi ametaja msimamo wa China kuhusu mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja kati ya Iran na Marekani kuwa chanya na kusema: "Siku zote China imekuwa na misimamo yenye kujenga na imeunga mkono mazungumzo yanayofanyika."
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran sanjari na kueleza kuwa, China imetangaza utayari wake wa kusaidia katika mchakato wa mazungumzo na kusema, nukta za kina kuhusiana na hilo zitafahamika katika safari hii.