China yaitaka Marekani iwe "mkweli" katika mazungumzo na Iran
Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya China ameitaka Marekani kuwa na ukweli wa kisiasa katika mazungumzo yake na Iran.
Lin Jian msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya China amebainisha kuwa, Marekani inapaswa kufanya mazungumzo yenye misingi ya kuheshimiana, na kuacha kutishia kutumia nguvu na mashinikizo ya kiwango cha juu kabisa.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China ameongeza kuwa: "Marekani ikiwa nchi ambayo ilijiondoa kwa upande mmoja katika Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA) na kuchangia mkwamo uliopo hivi sasa, inapaswa kuonyesha uaminifu wa kisiasa, kufanya mazungumzo na mashauriano yenye msingi wa kuheshimiana, na kuacha kutishia kutumia nguvu na mashinikizo ya kiwango cha juu kabisa."
Akigusia kuhusu kufanyika kikao cha pande tatu kati ya Iran, Russia na China mjini Moscow kuhusu suala la nyuklia la Iran amesema: "Beijing inaunga mkono mkutano huu na inauona kuwa ni hatua zaidi ya kuendeleza ufumbuzi wa kisiasa na kidiplomasia wa suala la nyuklia la Iran."
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China amebainishha kuwa, "Ningependa kusisitiza kwamba China inaamini kwa dhati kwamba kutatua suala la nyuklia la Iran kwa njia za kisiasa na kidiplomasia ndiyo njia pekee sahihi."
Mwanadiplomasia huyo mwandamizi wa China ameeleza kuwa, Beijing itaendelea kudumisha mawasiliano na uratibu na pande zote husika na kufanyia kazi utatuzi wenye uwiano ambao unashughulikia masuala halali ya pande zote.
Kadhalika amesema, katika hali ya sasa, pande zote zinazohusika zinapaswa kufanya juhudi za pamoja, kuimarisha mazungumzo na kutoa ushirikiano sambamba na kuzuia kuongezeka zaidi kwa mivutano.