Baqaei: Marekani na Magharibi zimehusika katika mauaji ya Israel ya waandishi wa habari huko Gaza
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Esmaeil Baqaei amesema kuwa, mwenendo wa utawala wa Israel wa kuwalenga waandishi wa habari wa Kipalestina umewezeshwa na msaada usiosita wa waungaji mkono wake wa Magharibi, hususan Marekani.
Akizungumza jana katika maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani, Baqaei alipongeza "ujasiri wa waandishi wa habari, wapiga picha na watayarishaji video ambao, katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, walihatarisha maisha yao ili kufichua ukatili wa mauaji ya kimbari ya kikoloni huko Wapalestina."
"Tunatoa heshima zetu kwa zaidi ya wafanyakazi 200 wa vyombo vya habari ambao wamekuwa wahanga wa kampeni ya mauaji ya kimbari waliyotaka kufichua," Baqaei alisema Jumamosi jana katika ujumbe wake kwenye mtandao wa X.
Alisema: "Waandishi hao wa habari walilengwa kwa sababu walihisi kuwajibika kuandika maumivu na mateso makali ya Wapalestina huko Gaza na kutangaza ukatili wa utawala vamizi na wa kibaguzi."
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran pia amesisitiza kwamba "mshirika wa Israel, Marekani na wenzake, wawezeshaji na wanaotetea ukatili wa Israel, wanahusika katika jinai hizo mbaya na watawajibishwa."

Mapema jana, Shirika la Wanahabari Wasio na Mipaka (RSF) lilitangazakuwa Palestina kwa sasa inatambuliwa kuwa eneo hatari zaidi duniani kwa wanahabari, kutokana na vita vya mauaji ya kimbari vya utawala wa Israel dhidi ya watu wa Gaza.
RSF imeripoti kuwa askari wa jeshi la Israel wamewaua karibu waandishi wa habari 200 katika miezi 18 ya kwanza ya vita hivyo, 42 kati yao wameuawa wakiwa kazini.