Msemaji wa serikali ya Iran: Vikwazo vya Marekani vinalenga maisha ya raia
(last modified Wed, 07 May 2025 06:34:41 GMT )
May 07, 2025 06:34 UTC
  • Msemaji wa serikali ya Iran: Vikwazo vya Marekani vinalenga maisha ya raia

Msemaji wa Serikali ya Iran amesema kuwa vikwazo vilivyowekwa na serikali ya Rais Donald Trump wa Marekani dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran vinaathiri maisha ya watu wa kawaida.

Bi Fatemeh Mohajerani alieleza haya jana mjini Tehran katika mkutano na waandishi wa habari na kukosoa vikwazo vya upande mmoja na vya kiholela vilivyoweka na serikali ya Trump tangu aingie madarakani mwezi Januari mwaka huku, sambamba na kuanza mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja kati ya Jamhuri ya Kiislamu na Marekani kuhusu miradi ya nyuklia ya nchi hii. 

"Hii si mara ya kwanza Iran inawekewa vikwazo; vikwazo hivi vinawalenga wananchi wa Iran na kuweka mashinikizo katika sekta ya matibabu ya wananchi, afya na maisha yao", amesema Mohajerani.

Msemaji wa Serikali ya Iran ameongeza kuwa, Tehran imechukua hatua zinazohitajika ili kukabiliana na vikwazo hivyo haramu. "Vikwazo dhidi ya Iran vinaashiria namna Marekani isivyoaminika katika suala la mazungumzo," amesema Bi Fatemeh Mohajerani.  

Msemaji wa Serikali ya Iran pia amegusia matamshi ya karibuni ya Marekani kuhusu kuizuia Iran kurutubisha madini ya urani na kukabiliwa na vikwazo vipya na kusema: Vikwazo vya Marekani ni vya upande mmoja, vya kiholela, na kinyume na sheria za kimataifa, na hatua hizi zinadhihirisha kuwa Marekani ni mkiukaji wa haki za binadamu na kielelezo cha gaidi wa kimataifa.