Iran: White House haiwezi kubadilisha ukweli kuhusu Jina la Ghuba ya Uajemi
(last modified Thu, 08 May 2025 11:06:52 GMT )
May 08, 2025 11:06 UTC
  •  Iran: White House haiwezi kubadilisha ukweli kuhusu Jina la Ghuba ya Uajemi

Ujumbe wa Iran katika Umoja wa Mataifa umelaani vikali jaribio lolote linaloweza kufanywa na Marekani kwa ajili ya kubadilisha jina la Ghuba ya Uajemi, na kusisitiza kwamba ukweli wa kihistoria hauwezi kubadilishwa kwa maamuzi ya kisiasa.

Kauli hiyo imekuja huku Rais Donald Trump wa Marekani, akitarajiwa kufanya safari Asia Magharibi (Mashariki ya Kati), ambapo ametangaza kwamba atatoa “habari muhimu” kuhusiana na ziara hiyo.

Masaa machache baada ya matamshi hayo, baadhi ya vyombo vya habari vya Magharibi vilidai kuwa tangazo hilo muhimu linahusiana na mpango wa serikali ya Marekani wa kubadilisha jina la Ghuba ya Uajemi.

Kwa mujibu Shirika la habari la IRNA, kufuatia kuenea kwa uvumi kuhusu mpango huo, Ujumbe wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Umoja wa Mataifa umetoa tamko kupitia mitandao ya kijamii ya “X,” na kusema:

“Kila mtu anapaswa kusimama dhidi ya upotoshaji ukweli. Uelewa wa historia na jiografia ni msingi wa utawala bora, na ukweli hauwezi kubadilishwa kwa maamuzi yanayofanyika katika Ofisi ya Oval (Ikulu ya White House).”

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran naye pia ametahadharisha kuhusu ghadhabu ya Wairani wote baada ya tetesi kwamba Rais Donald Trump wa Marekani ana mpango wa kubadili jina la Ghuba ya Uajemi katika ziara yake nchini Saudi Arabia, wiki ijayo.

Sayyid Abbas Araqchi jana alieleza kuwa ana imani kwamba Donald Trump anafahamu kuwa jina la Ghuba ya Uajemi linarejea nyuma karne kadhaa zilizopita na linatambuliwa na  wachora ramani na taasisi zote za kimataifa, na hata lilitumiwa na viongozi wote wa kanda hii katika mawasiliano yao rasmi hadi hivi karibuni katika muongo wa 60.

Araqchi amesema: "Hatua yoyote itakayochukuliwa katika uwanja huu haitakuwa halali au kuwa na taathira za kisheria na kijiografia, bali itawakasirisha Wairani wa matabaka yote na kuwa na taaathira za kisiasa hapa nchini, Marekani na duniani kote."

"Kinyume chake, hatua yoyote ya kisiasa ya kubadilisha jina lililoanzishwa kwa mujibu wa historia yaani jina la Ghuba ya Uajemi, inaashiria wazi nia ya uadui dhidi ya Iran na watu wake," amesema Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran.