Mafanikio ya Maendeleo ya Binadamu (HDI) ya Iran licha ya vikwazo
Iran imeorodheshwa miongoni mwa nchi zenye Kiwango cha Juu cha Maendeleo ya Binadamu katika Ripoti ya Maendeleo ya Binadamu ya 2025 ya Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP).
Ripoti hiyo inachambua maendeleo kwa kutumia viashiria vya Kiwango cha Maendeleo ya Binadamu (HDI) vinavyopima mafanikio katika afya, elimu na viwango vya kipato.
Kulingana na ripoti hiyo, HDI ya Iran inaendelea kuimarika na sasa nchi hii imeshika nafasi ya 75 kati ya nchi na maeneo 193 duniani kote. Hii inaipa Iran hadhi ya "Maendeleo ya Binadamu ya Juu".
Uboreshaji huu umetokea licha ya Iran kukabiliwa na vikwazo vikali vilivyowekwa na madola ya Magharibi vilivyoathiri watu wa kawaida, na kusababisha kupanda kwa bei ya bidhaa muhimu na makazi.
Kiwango cha Maendeleo ya Binadamu (HDI) ni miongoni mwa viashiria muhimu vya kupima maendeleo ya nchi.
Moja ya mafanikio muhimu baada ya Mapinduzi ya Kiislamu ya 1979 ni kuanzishwa kwa harakati ya kupambana na ujinga kwa agizo la mwanzilishi wa Jamhuri ya Kiislamu, Imam Khomeini, wakati zaidi ya nusu ya Wairani walikuwa hawajui kusoma na kuandika.
Ingawa Iran imepiga hatua katika nyanja zote kwa zaidi ya miaka 46, propaganda za Magharibi zimekuwa zikichora taswira ya Iran kama nchi yenye mateso na matatizo makubwa.
Sera za kijamii zilizotekelezwa hasa baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu zimepelekea HDI ya Iran kuimarika kwa kiwango kikubwa.
Mabadiliko kutoka sera za utawala wa kifalme wa Shah zilizolenga kuimarisha tabaka la wachache hadi kwenye sera za Mapinduzi ya Kiislamu za kuwapa fursa sawa watu waliotengwa zilijumuisha kupanua miundombinu na huduma za msingi kama umeme, maji safi, huduma za afya na elimu katika maeneo yote ya nchi kubwa ya Iran.
Upanuzi huu wa usawa wa huduma za afya na elimu ulipelekea kupungua kwa haraka kwa viwango vya umasikini, ambapo kiwango cha umasikini kilichokuwa asilimia 25 miaka ya 1970 kilishuka hadi chini ya asilimia 10 mwaka 2014.
Ripoti hiyo ya UNDP imeonesha matumaini makubwa kuhusu uwezo wa akili mnemba (AI), na imebainisha kwamba kasi ya ajabu ambayo zana za AI za bure au gharama ya chini zimekubaliwa na wafanyabiashara na watu binafsi imekuwa ya kushangaza. Ripoti hiyo inasisitiza jinsi Akili Mnemba inaweza kuleta msukumo mpya wa maendeleo.
Katika mustakabali, Iran ina uwezo wa kuunda fursa mpya za uwekezaji kwa kutumia akili mnemba kuendeleza ubunifu wa kisayansi na kiteknolojia.