Araqchi: Iran imo mbioni kuanzisha tena uhusiano na Bahrain na Misri
(last modified Tue, 20 May 2025 13:34:21 GMT )
May 20, 2025 13:34 UTC
  • Araqchi: Iran imo mbioni kuanzisha tena uhusiano na Bahrain na Misri

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamahuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, mchakato wa kurejesha uhusiano wa nchi hii na Bahrain na Misri umeanza.

Sayyid Abbas Araqchi amebainisha kwamba, maombi kadhaa yamefanywa kuanzisha uhusiano na Manama tangu Tehran na Riyadh zirekebishe uhusiano wao mnamo 2023.

Mwanadiplomasia huyo mkuu amesema juhudi zinaendelea za kurejesha uhusiano na taifa hilo la Kiarabu la Ghuba ya Uajemi, akielezea matumaini kwamba juhudi hizo zitazaa matunda hivi karibuni.

Kuhusu uhusiano wa Tehran na Cairo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amebainisha kuwa uhusiano kati ya Iran na Misri umepanuka kwa kiasi kikubwa.

Araqchi amesema, marais na mawaziri wa mambo ya nje wa nchi zote mbili wamekutana mara kadhaa na kudumisha mazungumzo ya simu mara kwa mara.

 Bahrain iliifuata Saudi Arabia kuvunja uhusiano wa kidiplomasia na Iran mnamo Januari 4, 2016, baada ya waandamanaji nchini Iran walioghadhibishwa na kunyongwa mwanazuoni mashuhuri wa madhehebu ya Shia Sheikh Nimr Baqir al-Nimr na serikali ya Saudia kuvamia jengo la ubalozi wa nchi hiyo hapa mjini Tehran.

Tehran na Riyadh zilifikia makubaliano katika mji mkuu wa China wa Beijing mwezi Machi 2023 kurejesha uhusiano wa kidiplomasia na kufungua tena balozi na ujumbe.

Juni mwaka jana Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Bahrain zilitoa taarifa ya pamoja zikielezea kuwekwa mikakati muhimu ya kuanzisha mazungumzo baina ya nchi mbili kwa lengo la kuchunguza namna ya kurejesha uhusiano wa kisiasa.