Mazungumzo ya Marais wa Iran na Russia mjini Baku Azerbaijan
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i12889-mazungumzo_ya_marais_wa_iran_na_russia_mjini_baku_azerbaijan
Marais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Russia wamekutana na kufanya mazungumzo mjini Baku Azerbaijan na kujadiliana kuhusiana na matukio ya kieneo na kimataifa.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 08, 2016 23:56 UTC
  • Mazungumzo ya Marais wa Iran na Russia mjini Baku Azerbaijan

Marais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Russia wamekutana na kufanya mazungumzo mjini Baku Azerbaijan na kujadiliana kuhusiana na matukio ya kieneo na kimataifa.

Marais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Vladimir Putin wa Russia waliokwenda Azerbaijan kushiriki mkutano wa pande tatu, walikutana pambizoni mwa mkutano huo ambapo mbali na kuzungumzia masuala ya pamoja ya Moscow na Tehran walibadilishana mawazo pia kuhusiana na masuala mbalimbali yanayojiri hivi sasa ulimwenguni.

Suala la kuimarishwa uhusiano wa pande mbili ni jambo lililopewa kipaumbele katika mazungumzo ya Marais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Russia huko mjini Baku Azerbaijan.

Kabla ya hapo Rais Rouhani mbali na kushiriki katika mkutano huo wa pande tatu alikutana na kufanya mazungumzo na viongozi mbalimbali wa Azerbaijan.

Marais wa Iran na Azerbaijan

Akizungumza katika kamati za juu za pande mbili mjini Baku akiwemo pia Rais Ilham Aliyev, Rais Hassan Rouhan alisema kuwa, ugaidi ni tishio kwa nchi zote na kwamba, ushirikiano wa nchi zote za eneo ikiwemo Azerbaijan unaweza kung'oa mizizi ya ugaidi na kurejesha amani na utulivu kamili katika eneo hili.

Rais Rouhani alisisitiza kwamba, ni jambo la kuchukiza kwa makundi ya kitakfiri kutekeleza ukatili huo nyuma ya pazia la Uislamu na kusisitiza kuwa, Uislamu ni dini ya amani, misimamo ya wastani na yenye kuhimiza juu ya kutendeana wema na haki.

Rais Hassan Rouhani

Rais Hassan Rouhani  wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran aliwasili jana Baku mji mkuu wa Azerbaijan kwa ziara rasmi nchini humo akiongoza ujumbe wa ngazi ya juu.

Hati sita za makubaliano ya ushirikiano kati ya Tehran na Baku zimesainiwa ikiwa ni katika fremu ya kuimarisha uhusiano na ushirikiano kati ya nchi mbili hizo.