Iran yalaani vikali hatua ya E3 kutekeleza "snapback", yasema haina uhalali kisheria
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imelaani vikali uamuzi uliochukuliwa na Ufaransa, Ujerumani na Uingereza siku ya Alkhamisi wa kuanzisha utaratibu wa "snapback" wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wa kurejesha papo kwa papo vikwazo vya baraza hilo dhidi yake kutokana na mpango wake wa nyuklia.
Waziri wa Mambo ya Nje Abbas Araghchi amesema hatua hiyo "si ya haki, ni haramu na haina msingi wowote wa kisheria" na kusisitiza kwamba Iran itatoa mjibizo ipasavyo ili kulinda haki na maslahi yake ya kitaifa.
Araghchi amekumbusha kuwa, mchakato wa 'snapback', ambayo ni hatua isiyoweza kupingwa kwa kura ya turufu ulioingizwa katika makubaliano ya nyuklia ya 2015 yanayojulikana kama JCPOA, ulianzishwa licha ya Iran kuendelea kufungamana na diplomasia na kuonyesha uwazi katika shughuli zake za nyuklia.
Kwa sababu hiyo, amesisitiza kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itatoa mjibizo unaostahiki kwa hatua hiyo isiyo na uhalali wa kisheria na ambayo haikuhitaji kuchukuliwa na nchi tatu za Ulaya, ili kulinda haki na maslahi yake ya kitaifa.
Nchi tatu zinazounda troika ya Ulaya, yaani Uingereza, Ufaransa na Ujerumani, kwa mashauriano na Mkuu wa Sera za Nje wa Umoja wa Ulaya, jana Alkhamisi ziliijulisha rasmi Iran kwa njia ya simu kuhusu nia yao ya kulitaarifu Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu kuanza mchakato wa "suluhisho la mzozano" kulingana na utaratibu wa JCPOA.
Hatua hii inaweka muda wa hadi siku 30 kabla ya kurejesha tena vikwazo vya Umoja wa Mataifa dhidi ya Iran, ambavyo vilisimamishwa tangu uliposainiwa mwaka 2015 mkataba wa nyuklia unaojulikana kama Mpango Kamili wa Utekelezaji wa Pamoja, JCPOA.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema anatumai nchi za Ulaya zitautafakari upya na kuubadili uamuzi wao huo…/