Iran: IAEA haina haki ya kutaka kukagua vituo vilivyoshambuliwa
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i134342-iran_iaea_haina_haki_ya_kutaka_kukagua_vituo_vilivyoshambuliwa
Mkuu wa shirika la nyuklia la Iran amekosoa wito wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki IAEA wa kufanya ukaguzi mpya kwenye maeneo ya nyuklia yaliyoshambuliwa, akisisitiza kwamba taasisi hiyo ya UN haina itifaki zilizo wazi za kukagua maeneo ambayo yalishambuliwa na utawala wa Israel na Marekani.
(last modified 2025-12-15T11:35:22+00:00 )
Dec 15, 2025 11:35 UTC
  • Iran: IAEA haina haki ya kutaka kukagua vituo vilivyoshambuliwa

Mkuu wa shirika la nyuklia la Iran amekosoa wito wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki IAEA wa kufanya ukaguzi mpya kwenye maeneo ya nyuklia yaliyoshambuliwa, akisisitiza kwamba taasisi hiyo ya UN haina itifaki zilizo wazi za kukagua maeneo ambayo yalishambuliwa na utawala wa Israel na Marekani.

Akizungumza na waandishi wa habari pambizoni mwa hafla ya kuzindua mafanikio ya hivi karibuni ya Taasisi ya Utafiti wa Sayansi na Teknolojia ya Nyuklia, Eslami amejibu matamshi ya hivi karibuni ya Mkurugenzi Mkuu wa IAEA Rafael Grossi kuhusu kuanza tena kwa ukaguzi nchini Iran.

Eslami amesema ukaguzi umefanywa katika vituo ambavyo havikushambuliwa, lakini amesisitiza kwamba suala muhimu sasa linahusu maeneo ya nyuklia ambayo yalishambuliwa kijeshi. Amesema kwamba ukaguzi wa vituo hivyo unahitaji itifaki iliyo wazi na iliyofafanuliwa.

"Shirika hilo, ambalo halijalaani [mashambulizi ya Israel na Marekani dhidi ya Iran mwezi Juni] na halina miongozo iliyowekwa, halina haki ya kudai linakusudia kufanya ukaguzi," Eslami amesisitiza.

Haya yanajiri huku Iran ikizindua mafanikio matatu ya kisasa katika sayansi ya nyuklia hii leo, ikiangazia maendeleo katika matumizi ya kimatibabu na utafiti pamoja na uzinduzi wa mtandao wa kitaifa wa nyuklia.

Hafla ya uzinduzi wa mafanikio hayo imefanyika mapema leo Jumatatu katika Kituo cha Maonyesho cha Kimataifa cha Tehran, ikihudhuriwa na Mohammad Reza Aref, Makamu wa Rais wa Iran, na Mohammad Eslami, Mkuu wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran.

Wakati wa hafla hiyo, Taasisi ya Utafiti wa Sayansi na Teknolojia ya Nyuklia imezindua kifaa cha uchunguzi wa mionzi, Gallium-68, kilichoundwa kwa ajili ya kupiga picha melanoma iliyoenea, kifaa cha matibabu cha mionzi, Lutetium-177, na kifaa kinachojiendesha kikamilifu kwa ajili ya kutibu maumivu ya mifupa.