Iran yaihutubu UN kuhusu 'mwenendo haramu endelevu' wa Trump
Iran imeuonya rasmi Umoja wa Mataifa kuhusu "mwenendo haramu endelevu" wa Marekani, kufuatia matamshi ya vitisho ya Rais Donald Trump ambayo Jamhuri ya Kiislamu imeyashutumu na kuyaeleza kama ya uingiliaji wa mambo yake ya ndani na tishio la wazi la utumiaji nguvu.
Katika barua iliyoandikiwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na wanachama wa Baraza la Usalama jana Ijumaa, Amir-Saeid Iravani, Balozi wa Kudumu wa Iran katika umoja huo, amesema kauli ya Rais wa Marekani iliyotolewa mapema jana ilikuwa "mfano mwingine dhahiri wa kuingilia kati masuala ya ndani ya nchi mwanachama wa Umoja wa Mataifa, kinyume na sheria ya kimataifa na hati ya Umoja wa Mataifa."
Iravani amesema kwenye barua hiyo kwamba, Trump ametishia waziwazi kutumia nguvu dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu, akitangaza kwamba Marekani "imejizatiti na iko tayari kuondoka," matamshi yanayoashiria kuchochea vurugu, machafuko, na vitendo vya kigaidi ndani ya nchi.
Wakati huo huo, Spika wa Bunge la Iran amejibu vitisho hivyo vya kijeshi vya Trump dhidi ya taifa la Iran akisema kwamba, kambi na vikosi vyote vya Marekani vitakuwa shabaha halali iwapo vitafanya kitendo chochote cha uvamizi. Mohammad-Bagher Ghalibaf amesisitiza kwamba, taifa hili litawakatisha tamaa maadui kama kawaida, akiongeza kuwa maandamano ya amani ya wafanyabiashara na wawekezaji yameruhusiwa na serikali ya Iran.
"Shetani amepaza sauti yake kwa sababu juhudi za watendaji wa huduma za ujasusi [za kigeni] kugeuza maandamano halali ya wafanyabiashara na wajasiriamali kuwa vita vya mijini vyenye vurugu na silaha, zilishindwa kutokana na kuwa macho taifa lenye uzoefu la Iran."
Huku hayo yakiripotiwa, Ubalozi wa Iran jijini London umelaani kile ulichokielezea kama matamshi ya kinafiki na ya uingiliaji kati kutoka kwa wabunge kadhaa wa Bunge la Uingereza kuhusu masuala ya ndani ya Iran, ukiwataka wajiepushe na kupotosha maoni ya umma.
Katika taarifa iliyochapishwa kwenye mtandao wa X jana Ijumaa, Ubalozi wa Iran ulisema matamshi hayo ni "ya kusikitisha na yasiyofaa." Umekosoa misimamo ya kinafiki ya wabunge wa Uingereza, ukiwashutumu kwa kuwa na hulka ya kuingilia masuala ya ndani ya nchi zingine.