Ripoti: Iran, Marekani kufanya mazungumzo ya nyuklia mjini Istanbul
-
Abbas Araghchi na Steve Witkoff
Iran na Marekani zinapanga kufanya duru mpya ya mazungumzo kuhusu mpango wa nyuklia wa Tehran.
Ripoti ya shirika la habari la Reuters imeeleza kuwa mazungumzo hayo yatafanyika Ijumaa ijayo katika mji wa Istanbul, Uturuki kati ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Abbas Araghchi na Steve Witkoff, Mjumbe Maalumu wa Rais wa Marekani.
Ripoti hiyo imewanukuu maafisa na wanadiplomasia ambao hawakutajwa majina yao kutoka Iran na Marekani wakisema kuwa wawakilishi kutoka Qatar, Saudi Arabia, Umoja wa Falme za Kiarabu na Misri pia watahudhuria mazungumzo hayo ambayo wamesema yatajumuisha mikutano ya pande mbili, pande tatu na pande kadhaa.
Mazungumzo hayo kati ya Iran na Marekani yameripotiwa ikiwa zimepita siku tatu baada ya Ali Larijani, Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran, kusema kuwa fremu ya mazungumzo ya nyuklia kati ya Iran na Marekani inaendelea kushughulikiwa na kutupilia mbali uvumi wa vyombo vya habari kuhusu uwezekano wa mashambulizi ya Marekani dhidi ya Iran.
Kauli hii ya Larijani ilifuatiwa haraka na matamshi ya Rais wa Marekani Donald Trump, ambaye alisema Iran imeanza kuwasiliana na nchi hiyo.
Hata hivyo hadi sasa hakuna taarifa yoyote kwa maafisa wa Iran kuhusu ripoti hii ya Reuters kwamba mazungumzo hayo yatafanyika Istanbul. Shirika la habari la Reuters limesema hayo masaa machache baada ya tovuti ya Axios ya Marekani kuchapisha taarifa inayofanana na hiyo ikidai kuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi, atakutana Ijumaa na Steve Witkoff Mjumbe Maalumu wa Rais wa Marekani siku ya mjini Istanbul mjini Istanbul.
Iran imetahadharisha kuwa itatoa jibu kali hata kwa hatua ndogo ya kijeshi ya Marekani dhidi ya ardhi yake.