Shamkhani: Mazungumzo ya Marekani yanaweza kuzaa matunda iwapo tu yataonyesha heshima, mantiki
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i136208-shamkhani_mazungumzo_ya_marekani_yanaweza_kuzaa_matunda_iwapo_tu_yataonyesha_heshima_mantiki
Afisa wa ngazi ya juu wa Iran amesema kuwa mazungumzo yajayo ya nyuklia na Marekani yanaweza kuwa na tija iwapo tu yatajiepusha na anga ya vitisho na madai yasiyo na mantiki, na kusisitiza kuwa Tehran haina nia ya kuhamisha nje ya nchi akiba yake ya urani iliyorutubishwa chini ya makubaliano yoyote.
(last modified 2026-02-03T09:36:48+00:00 )
Feb 03, 2026 08:10 UTC
  • Admeri Ali Shamkhani
    Admeri Ali Shamkhani

Afisa wa ngazi ya juu wa Iran amesema kuwa mazungumzo yajayo ya nyuklia na Marekani yanaweza kuwa na tija iwapo tu yatajiepusha na anga ya vitisho na madai yasiyo na mantiki, na kusisitiza kuwa Tehran haina nia ya kuhamisha nje ya nchi akiba yake ya urani iliyorutubishwa chini ya makubaliano yoyote.

Admeri Ali Shamkhani, Mjumbe wa Baraza Kuu la Ulinzi ambaye pia ni Mshauri wa Ayatullah Sayyid Ali Khamenei Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameeleza haya katika mahojiano ya kina na Televisheni ya Al-Mayadeen yenye makao yake nchini Lebanon. 

"Iwapo mazungumzo yataanza chini ya masharti niliyotaja, kuepuka vitisho na kujiepusha na amri zisizo na mantiki, basi bila shaka kuna uwezekano wa mikutano ya moja kwa moja na isiyo ya moja kwa moja na upande wa Marekani,” amesema Ali Shamkhani.

Admeri Ali Shamkhani ameeleza haya kufuatia ripoti kwamba Steve Witkoff, Mjumbe Maalumu wa Rais Donald Trump wa Marekani, na Abbas Araghchi Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran wanarajiwa kukutana Ijumaa hii mjini Istanbul, Uturuki. 

Katika mahojiano hayo na televisheni ya al Mayadeen, Ali Shamkhani ameonekana akiwa amevalia sare za kijeshi kama ishara ya kuwa tayari, huku akipuuzilia mbali uvumi kwamba Iran inaweza kuhamisha madini yake ya urani nje ya nchi.

Amesisitiza kuwa shughuli za nyuklia za Iran ni za amani na zinasimamiwa ndani ya nchi. 

Ameongeza kuwa urutubishaji wetu wa urani wa asilimia 60 unaweza kupunguzwa hadi asilimia 20 iwapo kuna wasiwasi wa kweli, lakini lazima na wao watupe kitu mkabala wake.