Iran yasema “tamaa isiyo na mwisho ya Marekani haina mipaka”
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i138170-iran_yasema_tamaa_isiyo_na_mwisho_ya_marekani_haina_mipaka
Iran imesema kuwa Marekani haijaacha mwenendo wake wa madai kupita kiasi na tamaa isiyo na kikomo, ikithibitisha kuwa imepokea jibu la watawala wa Washington kuhusu pendekezo la Iran la mpango wa pointi 14 unaohusu mazungumzo ya pande zote, yenye lengo la kusitisha vita dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu.
(last modified 2026-05-05T05:33:58+00:00 )
May 05, 2026 05:30 UTC
  • Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Esmaeil Baghaei
    Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Esmaeil Baghaei

Iran imesema kuwa Marekani haijaacha mwenendo wake wa madai kupita kiasi na tamaa isiyo na kikomo, ikithibitisha kuwa imepokea jibu la watawala wa Washington kuhusu pendekezo la Iran la mpango wa pointi 14 unaohusu mazungumzo ya pande zote, yenye lengo la kusitisha vita dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu.

Akizungumza katika mkutano wake wa kila wiki na waandishi wa habari siku ya Jumatatu, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Esmaeil Baghaei, amesema kuwa Iran imepokea jibu la Marekani kupitia wapatanishi wa Pakistan na kwa sasa inalifanyia tathmini, lakini hakutoa maelezo mahsusi kuhusu yaliyomo kwenye jibu hilo.

Ameongeza kuwa: “Marekani inaendelea na tabia yake ya tamaa ya kudumu na madai yasiyo na mipaka. Tunakabiliana na upande unaobadilisha misimamo yake mara kwa mara, jambo ambalo linafanya mchakato wowote wa kidiplomasia kuwa mgumu zaidi.”

Baghaei amepinga uvumi ulioripotiwa na baadhi ya vyombo vya habari kuhusu masuala ya nyuklia, akisema kuwa uvumi huo umetokana na majadiliano ya awali ambayo yalihusisha tu suala la nyuklia.

Amesisitiza kuwa mazungumzo kuhusu urutubishaji na urani ni dhana tu. “Katika hatua hii, hatuzungumzii chochote kingine isipokuwa kusitishwa kabisa kwa vita.”

Aidha amebaini kuwa Iran itatangaza msimamo wake baada ya kufikia hitimisho, tena kupitia Pakistan ambayo ni mpatanishi.

Baghaei pia amesema kuwa Iran itachukua maamuzi muhimu kuhusu mwelekeo wa hatua zake katika siku zijazo.

Katika mahojiano ya televisheni siku ya Jumapili, Baghaei alifafanua kuwa pendekezo la Iran linajikita kikamilifu katika kusitisha uchokozi wa Marekani na Israel dhidi ya Iran pamoja na mapigano katika eneo la Asia Magharibi.

Akiitaja Iran kama taifa la mwambao wa Mlango wa Hormuz, aliongeza kuwa Iran imeandaa mikakati inayolingana na sheria za kimataifa ili kuhakikisha kuwa hakuna uchokozi unaofanywa dhidi ya maslahi ya taifa—akisisitiza kuwa hili ni kanuni inayokubalika kimataifa.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Abbas Aragchi pia amesisitiza kuwa kwa sasa Iran haifanya mazungumzo ya nyuklia na tawala hasimu. Ameyasema hayo Jumatatu alipokuwa katika kikao cha faragha za Kamati ya Usalama wa Taifa na Sera a Kigeni katika Bunge la Iran.