Spika Qalibaf: Iran inamrudisha nyuma adui kupitia umoja wa kitaifa
-
Mohammad Baqir Qalibaf
Mohammad Baqir Qalibaf Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran (Bunge) amesema kuwa Iran, kupitia umoja wa kitaifa, inamrudisha nyuma adui katika vita vinavyoacha historia.
Spika Qalibaf alieleza hayo jana Jumapili wakati jitihada za upatanishi za Pakistan zikiendelea na kuzielekeza Tehran na Washington kwenye kukamilisha hati ya mamapatano yenye lengo la kuhitimisha hujuma haramu ya Marekani na Israel dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu.
"Tunamrudisha nyuma adui katika vita vikubwa na vya kihistoria. Kama Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu alivyosisitiza, jambo muhimu zaidi katika ushindi kwenye vita hivi ni mshikamano na umoja wa wananchi," amesema Spika wa Bunge la Iran.
Ameongeza kuwa, "jambo lililomrudisha nyuma adui, sambamba na nguvu za jeshi na utayarifu wa kulinda na kuihami nchi wa vikosi vya ulinzi, ni uimara na umoja wa wananchi mbele ya adui mkubwa; siri hii ya ushindi lazima ilindwe.
Mohammad Baqir Qalibaf pia amemshukuru Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Sayyid Mojtaba Khamenei, kwa ujumbe wake wa kistratejia na wa kutia moyo kwa wabunge wa Iran, akisema utatumika kama ramani ya Bunge na mwanga wa uongozi wa siku zijazo.
Wakati huo huo, Qalibaf ameonya kuhusu chokokocho za adui za kutaka kuzusha hitilafu miongoni mwa wananchi wa Iran kupitia mashinikizo ya kiuchumi na kupotosha vyombo vya habari ili kufidia kushindwa kwake kijeshi na kuilazimisha Jamhuri ya Kiislamu isalimu amri.