Rais wa Venezuela safarini Iran kwa mazungumzo ya mafuta
(last modified Sat, 22 Oct 2016 04:26:22 GMT )
Oct 22, 2016 04:26 UTC
  • Rais wa Venezuela safarini Iran kwa mazungumzo ya mafuta

Rais Nicolas Maduro wa Venezuela anaitembelea Iran katika sehemu ya safari yake ya kuzitembelea nchi zinazozalisha mafuta kwa wingi duniani ili kujaribu kuleta uthabiti katika soko la kimataifa la mafuta.

Maduro anatazamiwa kuwasili Tehran hii leo Jumamosi ambapo atafanya mazungumzo na Rais Hassan Rouhani wa Iran. Rais wa Venezuela alianza safari yake hiyo ya siku nne kwa kuitembelea Saudi Arabia Alhamisi na mbali na Iran atatembelea pia Qatar na Jamhuri ya Azerbaijan.

Akizungumza kabla ya kuanza safari yake hiyo, Maduro amesema lengo la safari yake hiyo ni kuhakikisha bei ya mafuta inapanda hatua kwa hatua ili kuleta uthabiti katika masoko ya kimataifa.

Katika mkutano wa Jumuiya ya Nchi Zinazouza Mafuta kwa Wingi Duniani OPEC nchini Algeria Septemba 28, nchi wanachama waliafiki kupunguza kiwango cha uzalishaji ili kuongeza bei ya mafuta ghafi katika soko la kimataifa. Nchi hizo zinatazamiwa kukutana tena Novemba 30 ili kukamilisha mapatano hayo.

Hata hivyo Iran haitapunguza uzalishaji wake kwa sababu ilikuwa tayari imeshapunguza katika miaka ilimokuwa chini ya vikwazo vya kimataifa. Iran, ambayo ni mzalishaji mkubwa katika OPEC baada ya Saudi Arabia na Iraq, imekuwa ikiongeza uzalishaji wa mafuta yake ili kufikia kiwango cha kabla ya vikwazo na hivyo inapinga shinikizo la kuitaka ipunguze uzalishaji.

 

Tags