Iran yaishukuru Kenya kwa kuwaachia huru raia wake waliokamatwa kimakosa
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeishukuru serikali ya Kenya kwa kuwaachia huru mawakili wawili raia wa nchi hii waliokamatwa kimakosa na polisi katika mji mkuu Nairobi, wiki mbili zilizopita.
Bahram Qassemi, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ameishukuru serikali na vyombo vya mahakama vya nchi hiyo ya Afrika Mashariki, kwa ushirikiano wao kuhusiana na kadhia ya kukamatwa mawakili hao.
Kwa mujibu wa Qassemi, Iran ilituma ujumbe wa kidiplomasia nchini Kenya kwenda kufuatilia suala hilo, na sasa mawakili hao wameachiwa huru na kurejea nchini.
Kufuatia taarifa za kukamatwa raia hao Wairani nchini Kenya, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran alitoa taarifa na kusema: "Mabwana Dkt. Abdul Hussein Safai na Dkt. Sayyed Nasrullah Ibrahimi ni mawakili rasmi wa Mahakama ya Iran na ambao pia ni wahadhiri wa vyuo vikuu na walitumwa Nairobi na familia za Wairani wawili waliofungwa jela nchini Kenya ili wafuatilie kesi zao na kutoa ushauri wa kisheria kwa wafungwa hao wawili.
Mawakili hao walikamatwa na polisi ya Kenya wakati wakirejea kutoka kuwatembelea wafungwa hao wa Kiirani.
Vyombo vya habari nchini Kenya viliripoti kuwa, wawili hao walikamatwa eti kwa kupiga picha ubalozi wa utawala haramu wa Israel jijini Nairobi. Mawakili hao pamoja na dereva wao walikamatwa wakiwa kwenye gari la ubalozi wa Iran jijini Nairobi Novemba 29.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran alisema mawakili hao Wairani walikamatwa kutokana na 'uingiliaji wa upande wa tatu' na kwamba uingiliaji huo ulilenga kuharibu uhusiano mzuri wa Iran na Kenya.