Mottaki: Umoja wa Waislamu unawatia kiwewe maadui
(last modified Sat, 07 Jan 2017 07:17:08 GMT )
Jan 07, 2017 07:17 UTC
  • Mottaki: Umoja wa Waislamu unawatia kiwewe maadui

Naibu Mkuu wa Jumuiya ya Kimataifa ya Kuyakurubisha Pamoja Madhehebu za Kiislamu katika masuala ya Iran amesema umoja na mshikamano wa Waislamu umewakosesha usingizi maadui wa dini hii tukufu.

Manouchehr Mottaki, Naibu Mkuu wa Jumuiya ya Kimataifa ya Kuyakurubisha Pamoja Madhehebu za Kiislamu aliyasema hayo jana katika mji wa Iranshahr, mkoa wa Sistan-Baluchestan hapa nchini, wakati wa hafla za mahafali za wanafunzi karibu 400 wa Kisunni, waliofuzu na kutunukiwa shahada mbali mbali.

Mottaki ameutaka ulimwengu wa Kiislamu kuwa macho na njama za maadui wanaojaribu kuzusha fitina na kupanda mbegu za mifarakano na migawanyiko kwa misingi ya madhehebu. Amesisitiza kuwa, Uislamu ni dini ya upendo, amani, umoja na udugu na wala sio dini ya migogoro na migawanyiko.

Maandamano ya kulaani kushtadi chuki dhidi ya Waislamu

Naibu Mkuu wa Jumuiya ya Kimataifa ya Kuyakurubisha Pamoja Madhehebu za Kiislamu amefafanua kuwa, umoja wa Waislamu ndio ufunguo wa ushindi katika masuala yao sambamba na kuzipatia ufumbuzi changamoto zao.

Amewatadharisha Waislamu kote duniani kutoingia katika mtego wa maadui wa dini hii tukufu, hususan njama za adui Marekani na utawala wa Kizayuni.

Manouchehr Mottaki, ambaye amewahi kuwa Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran ameongeza kuwa, ajenda na stratejia kuu inayotumiwa na maadui wa Uislamu hivi sasa ni kueneza hofu na chuki dhidi ya Uislamu na wafuasi wa dini hiyo tukufu.