Jan 10, 2017 08:20 UTC
  • Kiongozi Muadhamu aongoza Swala ya maiti ya Ayatullah Rafsanjani

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullahil Udhmaa Ali Khamenei ameongoza Swala ya maiti ya marehemu Ayatullah Akbar Hashemi Rafsanjani, rais wa zamani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Umati mkubwa ukiongozwa na viongozi wa ngazi za juu wa serikali na wanazuoni wameshiriki Swala hiyo, iliyoswaliwa katika Chuo Kikuu cha Tehran.

Takriban viongozi wote wa ngazi za juu wa Iran akiwemo Rais Hassan Rouhani, Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran), Ali Larijani na Mkuu wa Vyombo vya Mahakama Ayatullah Sadeq Amoli Larijani wameshiriki katika swala hiyo. 

Kiongozi Muadhamu na viongozi wengine wa ngazi za juu wa Iran wakimuombea dua marhum Rafsanjani

Shughuli ya kusindikiza mwili wa marehemu Ayatullah Rafsanjani ilianza saa nne asubuhi ikiongozwa na Rais Hassan Rouhani, mawaziri wa serikali na maafisa wa ngazi za juu wa jeshi wakifuatiwa na wananchi katika Husainiya ya Jamaran. Mwili wa marehemu Ayatullah Rafsanjani utazikwa kandokando ya kaburi la mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu, Imam Ruhullah Khomeini katika eneo al Behest Zahraa katika viunga vya mjini Tehran.

Ayatullah Akbar Hashemi Rafsanjani aliyekuwa Mkuu wa Halmashauri ya Kuainisha Maslahi ya Mfumo wa Kiislamu wa Iran alifariki dunia Jumapili usiku kutokana na matatizo ya moyo.

Tags