Jan 10, 2017 16:42 UTC
  • Rais wa Russia atuma salamu za rambirambi kwa kifo cha Ayatullah Rafsanjani

Rais Vladimir Putin wa Russia ametuma salamu za rambirambi na mkono wa pole kufuatia kifo cha Ayatullah Hashemi Rafsanjani, Mkuu wa Halmashauri ya Kuainisha Maslahi ya Mfumo wa Iran.

Mehdi Sanai, Balozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nchini Russia ameeleza kupitia ukurasa wake wa kijamii wa Telegram kuwa: "Rais Vladimir Putin wa Russia ametoa mkono wa pole kwa wananchi na serikali ya Iran kutokana na kifo cha Ayatullah Hashemi Rafsanjani."

Leo asubuhi, mwakilishi maalumu wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia alifika ubalozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mjini Moscow na kutoa mkono wa pole kufuatia kifo cha Sheikh Hashemi Rafsanjani.

Marehemu Ayatullah Hashemi Rafsanjani

Kuanzia leo, kitabu cha kumbukumbu cha maombolezo ya Ayatullah Hasehmi Rafsanjani kimefunguliwa katika ubalozi wa Iran mjini Moscow kwa ajili ya kupokea salamu za rambirambi, mkono wa pole na maoni ya wasifu wa shakhsia huyo yanayotolewa na maafisa na shakhsia mbalimbali wa Russia na wa kigeni.

Mwanadiplomasia akisaini kitabu cha maombolezo

Wakati huohuo mabalozi wa Iraq, Mongolia, Bosnia Herzegovina, Palestina, Ugiriki, Lithuania, Burkina Faso, Syria, Jordan, Oman pamoja na maafisa kadhaa wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia na shakhsia tofauti wa kisiasa wa nchi hiyo wamefika kwenye ubalozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mjini Moscow ili kutoa mkono wa pole kwa serikali na wananchi wa Iran kutokana na kifo cha Ayatullah Hashemi Rafsanjani…/

 

Tags