Jan 20, 2017 04:28 UTC
  • Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu
    Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, ametoa ujumbe wa maombolezo kufuatia kuwaka moto na kuporomoka jengo la kibiashara la Plasco katikati ya Tehran na kuwapa mkono wa pole wafiwa wote na kuwataka maafisa husika kufanya juhudi zao zote kuhakikisha watu waliokwama kwenye jengo hilo wanaokolewa.

Katika sehemu moja ya ujumbe wake huo, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema, ujasiri na kujitolea maafisa wa zimamoto katika operesheni ya kuwaokoa watu na kupelekea wenyewe kupata ajali ya hatari wakati wakitekeleza majukumu yao kwa kujitolea kikamilifu ni jambo ambalo limeujaza moyo wangu majonzi na huzuni kubwa lakini pia natoa pongezi zangu nyingi kwa hamasa iliyooneshwa na mashujaa hao.

Vile vile Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa, inabidi juhudi zote hivi sasa zielekezwe kwenye kuwaokoa watu waliokwama ndani ya jengo hilo na suala la kufuatilia sababu za ajali hiyo lifanyike baadaye.

Maafisa wa zimamoto wa Iran wakiendelea na operesheni ya kuwatoa watu waliokwama kwenye jengo la Plasco lililowaka moto na kuporomoka katikati ya jiji la Tehran Alkhamisi Januari 19, 2017

 

Naye Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ametoa ujumbe kufuatia tukio hilo la kusikitisha la kuungua moto na kuporomoka jengo hilo la ghorofa 17 na kupelekea makumi ya watu kujeruhiwa na kupoteza maisha.

Katika sehemu moja ya ujumbe wake huo, Rais Hassan Rouhani amesema, ijapokuwa ajali ya kusikitisha ya kuwaka moto na kuporomoka jengo la Plasco la mjini Tehran ni tukio chungu lenye kusikitisha, lakini hamasa iliyooneshwa na wafanyakazi wa zima moto imeonesha ushujaa na moyo wao mkubwa wa kujitolea katika kuhudumia watu na jambo hilo limelitumbukiza taifa zima la Iran kwenye majonzi na huzuni kubwa.

Jana asubuhi, jengo la ghorofa 17 la la kibiashara la Plasco lililokuweko kwenye barabara ya Jomhuriye Islami katikati ya Tehran liliwaka moto na baadaye kuporomoka wakati wafanyakazi wa zima moto walipokuwa katika jitihada za kuzima moto huo. Meya wa jiji la Tehran, Mohammad Baqer Qalibaf awali alinukuliwa akisema, wafanyakazi 20 wa zimamoto wamepoteza maisha kwenye ajali hiyo.

Tags