Rouhani: NAM iungane dhidi ya misimamo mikali ya upande mmoja
(last modified Thu, 09 Feb 2017 07:30:14 GMT )
Feb 09, 2017 07:30 UTC
  • Rouhani: NAM iungane dhidi ya misimamo mikali ya upande mmoja

Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ametoa wito wa kuwepo ushirikiano zaidi baina ya nchi wananchama wa Jumuiya ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote NAM, akisisitiza kuwa mataifa huru yanafaa kuungana dhidi ya madola yenye kupenda kutoa maamuzi ya upande mmoja na misimamo ya kuchupa mipaka.

Rais Rouhani aliyasema hayo jana Jumatano alipokutana na kufanya mazungumzo na Delcy Rodriguez, Waziri wa Mambo ya Nje wa Venezuela na mwenzake wa Mafuta Nelson Martinez hapa mjini Tehran na kuongeza kuwa, mataifa huru na hususan nchi wanachama wa Jumuiya ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote NAM yanafaa kufanya kazi bega kwa bega na kushirikiana kwa shabaha ya kuwa na ushawishi mkubwa katika masuala ya eneo na kimataifa.

Dakta Rouhani amefafanua kuwa: "Kutokana na hali ilivyo sasa, dunia inahitaji fikra, mawazo na mchango wa mataifa huru na jumuiya kama NAM, ili kutokomeza maamuzi ya upande mmoja yanayochukuliwa na baadhi ya madola, misimamo ya kufurutu ada, jinai na machafuko yanayoshuhudiwa katika pembe mbali mbali za dunia."

Mkutano wa NAM Septemba 2016

Itakumbukwa kuwa, akizungumza katika mkutano wa 17 wa NAM katika kisiwa cha Margarita nchini Venezuela Septemba mwaka jana 2016, Rais Rouhani alisema hivi sasa, kuliko wakati mwingine wowote ule, wanachama wa NAM wanahitaji mshikamano na ushirikiano na kusisitiza kuwa NAM ni kundi ambalo wanachama wake ni karibu robo tatu ya wanachama wote wa Umoja wa Mataifa na kwa hivyo nchi hizo zina nafasi isiyopingika katika kutatua matatizo ya sasa duniani. 

Kwa sasa harakati ya NAM ipo chini ya uenyekiti wa Venezuela, baada ya kukabidhiwa wadhifa huo wa mzunguko na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Septemba 2016.

Tags