Zarif: Saudia inachochea machafuko Mashariki ya Kati
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Mohammad Javad Zarif amesema Saudi Arabia inalenga kuchochea ghasia na machafuko Mashariki ya Kati.
Akizungumza mjini Tehran Jumamosi katika kikao cha waandishi habari akiwa amendamana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Malta George Vella, Zarif amesema: "Baadhi ya nchi katika eneo letu, hasa serikali ya Saudia zimekuwa zikifuatilia sera mbovu zenye lengo la kuibua ghasia na machafuko katika eneo lote."
Amesema sera kama hizo zinaufurahisha utawala haramu wa Israel na kupelekea kuenea chuki katika nchi za Kiarabu.
Zarif aidha amelaani hatua ya hivi karibuni ya Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi ya kuitaja haraki ya Hizbullah ya Lebanon kuwa kundi la kigaidi.
"Hezbollah ni harakati pekee ambayo imelinda mipaka ya Lebanon wakati wa uvamizi wa utawala wa Kizayuni wa Israel," amesema Zarif.
Zarif amesisitiza pia umuhimu wa mazungumzo na ushirikiano wa nchi za eneo ili kuzuia kuenea machafuko.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameonya kuwa Umoja wa Ulaya, Malta ikiwemo, unakabiliwa na misimamo mikali na ugaidi kutokana na wimbi la wakimbizi wanaoingia Ulaya.