Mar 28, 2017 16:21 UTC
  • Iran, Algeria kutumia tamaduni kukabili utakfiri na misimamo mikali

Waziri wa Utamaduni wa Algeria amesema harakati za kitamaduni zina nafasi chanya katika vita dhidi ya magenge ya utakfiri na yenye misimamo ya kufurutu ada.

Azzeddine Mihoubi, Waziri wa Utamaduni wa Algeria ameyasema hayo katika mazungumzo yake na mwenzake wa Iran mjini Algiers, Reza Salehi-Amiri na kuongeza kuwa, nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika inaitazama Jamhuri ya Kiislamu kama rafiki wa dhati ambaye wamesimama pamoja kidete dhidi ya makundi ya ukufurishaji.

Mihoubi amebainisha kuwa, Algiers na Tehran tayari zimepiga hatua za maana katika kuimarisha uhusiano wa pande mbili katika nyuga za uchumi na kisiasa na kusisitiza kuwa, kuna haja kwa nchi mbili hizi kuhakikisha kuwa zinaboresha mahusiano yao ya kitamaduni, haswa katika kipindi hiki cha fitina za makundi ya kigaidi na kitakfiri.

Waziri wa Utamaduni wa Iran

Waziri huyo kadhalika ameipongeza Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa kuwa mwenyeji wa mkutano wa Wiki ya Utamaduni ya Algeria katikati ya mwezi Disemba mwaka jana 2016.

Kwa upande wake, Waziri wa Utamaduni wa Iran, Reza Salehi-Amiri amesisitiza kuwa, Tehran na Algiers zinaweza kuimarisha uhusiano wao wa kitamaduni katika nyanja za senema, muziki na sanaa ya maonyesho na tamthilia.

Baada ya kuitembelea Algeria, Waziri wa Utamaduni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa sasa yuko katika ziara ya kuitembelea Tunisia, nchi nyingine ya kaskazini mwa Afrika.

Ramani ya Algeria

 

  

Tags