Iran na Kenya kuimarisha uhusiano wa kiuchumi
Balozi wa Iran nchini Kenya amesisitiza kuhusu kuimarishwa uhusiano wa kiuchumi baina ya Tehran na Nairobi.
Hadi Farajvand balozi wa Iran nchini Kenya ameyasema leo Jumamosi mjini Shiraz kusini mwa Iran pembizoni mwa kongamano la kuarifisha fursa za kibiashara nchini Kenya.
Dkt. Farajvand ameongeza kuwa, uhusiano wa Kenya na Iran umekuwa mzuri katika kipindi chote cha historia na kuongeza kuwa: "Inawezekana kuongeza kiwango cha mauzo ya Iran nchini Kenya kufika dola milioni 150-200 kwa mwaka."
Aidha amesema wanaharakati wa kiuchumi na wawekezaji Wairani wanaweza kuuza bidhaa mbali mbali nchini Kenya kama vile lami, vifaa vya ujenzi, mazulia n.k. Aidha amesema wawekezaji Wairani wanaweza kukodi ardhi nchini Kenya na kujihusisha na kilimo katika ardhi za nchi hiyo zenye rotuba.
Balozi Farajvand hali kadhalika amesema kuna usalama mzuri kwa wawekezaji nchini Kenya na kwamba nchi hiyo ya Afrika Mashariki ina mazingira mazuri kwa ajili ya wawekezaji.
Balozi huyo amesema wiki hii kutafanyika makongamano mengine ya kuarifisha fursa za kibiasahra nchini Kenya kwa wawekezaji Wairani. Makongamano hayo yanatazamiwa kufanyika katika miji ya Isfahan na Arak kati mwa Iran.