Rouhani: Iran haitachukua idhini kwa yeyote kuunda makombora na ndege
(last modified Sat, 15 Apr 2017 14:00:08 GMT )
Apr 15, 2017 14:00 UTC
  • Rouhani: Iran haitachukua idhini kwa yeyote kuunda makombora na ndege

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema nchi hii imekuwa muathirika wa hujuma ya kiuoga na kwa msingi huo haitachukua idhini kutoka kwa yeyote katika kuimarisha vikosi vyake vya ulinzi hasa uundaji wa makombora na ndege za kivita.

Rais Hassan Rouhani ameyasema hayo leo mjini Tehran katika sherehe ya kuziduliwa mafanikio ya Wizara ya Ulinzi ya Iran na kuongeza kuwa kuimarishwa misingi ya kujihami ya vikosi vya kijeshi vya Iran ni kwa ajili ya kujihami tu na wala si kwa ajili ya kuvamia nchi yoyote ile.

Rais Rouhani amebainisha kuwa ni jambo la dharura kuleta mlingano katika eneo na kuhifadhi uwezo wa Iran kuzuia hujuma ya adui jambo ambalo linahatarisha maslahi ya madola makubwa ya kibeberu na wakati huo huo kuwafikishia walimwengu ujumbe wa uadilifu na uhuru.

Rais wa Iran ameashiria hujuma kadhaa ambazo zimetekelezwa na baadhi ya nchi za eneo na madola makubwa hasa Marekani katika eneo la Mashariki ya Kati na kusema: "Uingiliaji wa madola makubwa na donda sugu la saratani, yaani utawala wa Israel ni jambo ambalo daima limekuwa chanzo cha wasiwasi na ukosefu wa amani Mashariki ya Kati."

Rais Rouhani ambaye pia ni mwenyekiti wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa Iran ameongeza kuwa: "Iran kamwe haijawahi kuwa na nia ya kuwahujumu wengine, haina na wala haitakuwa na nia hiyo." Hata hivyo amesisitiza umuhimu wa nchi hii kuchukua tahadhari kwani baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu mwaka 1979, imehujumiwa kisiasa, kijeshi na kiuchumi.

Rais Rouhan akizindua kombora la Anga kwa Anga la Fakkur

Rais Rouhani amesema hatua ya Iran kuweza kumiliki makombora wakati wa zama za vita vya kulazimishwa ilikuwa ni kwa mujibu wa takwa la taifa. Ameongeza kuwa, 'Taifa la Iran leo linajifakharisha kwa ajili ya Amiri Jeshi Mkuu, sekta ya viwanda, na vikosi vyake vya ulinzi."

Rais Rouhani pia ameashiria mafanikio ya miradi kadhaa ya kiulinzi nchini Iran na kusema: "utengenezaji wa ndege, helikopta, vifaru, magari ya deraya unaofanywa na wataalamu wa ndani ya nchi ni jambo la fakhari kubwa."

Katika sherehe hiyo ya leo, Rais Rouhani alizindua ndege ya kivita ya kutoa mafunzo ambayo imetengenezwa na wataalamu wa hapa nchini ambayo imepewa jina la Kauthar, drone ya upelelezi na yenye uwezo wa kusheheni silaha inayojulikana kama Muhajir 6, kombora la cruise liitwalo Nasir na kombora la anga kwa anga la Fakkur.