Iran yalaani shambulio la kigaidi na umwagaji damu mjini Paris
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imelaani shambulio la ufyatuaji risasi lililofanywa na kundi la kigaidi la Daesh mjini Paris, Ufaransa siku chache kabla ya kufanyika uchaguzi wa Rais nchini humo na imetoa wito kwa nchi mbalimbali kushikamana na kusaidia juhudi za kutokomeza tishio la ugaidi kwa azma thabiti.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Bahram Qassemi amesema katika taarifa iliyotolewa hii leo kuwa, uungaji mkono wa Magharibi kwa magaidi watenda jinai na mienendo yao ya kindumakuwili katika kushughulikia tatizo la ugaidi imewatia hamasa magaidi kuteleleza shambulio jingine barani Ulaya.

Qassemi ameutaja ugaidi kuwa ni tishio la kubwa zaidi kwa amani, utulivu na usalama wa dunia na kusisitiza kwamba, tatizo hilo haliwezi kupatiwa ufumbuzi bila ya kuwepo mwafaka na azma kubwa na ya kweli miongoni mwa wanachama wa jamii ya kimataifa.
Jana jioni mafisa wawili wa polisi ya Ufaransa waliuliwa kwa kupigwa risasi na wengine wawili kujeruhiwa vibaya mjini Paris katika shambulio lililodaiwa kufanywa na kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh.