Araqchi: Mazingira yaliyojengwa na serikali ya Trump kuhusiana na JCPOA hayakubaliki
(last modified Wed, 26 Apr 2017 02:33:13 GMT )
Apr 26, 2017 02:33 UTC
  • Araqchi: Mazingira yaliyojengwa na serikali ya Trump kuhusiana na JCPOA hayakubaliki

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema serikali mpya ya Marekani imejenga anga na mazingira ya utata, shaka na mkanganyo kuhusiana na hatima ya makubaliano ya nyuklia yanayojulikana kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA).

Sayyid Abbas Araqchi, ambaye pia ni Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran anayehusika na masuala ya sheria na kimataifa ameyasema hayo pembeni ya kikao cha saba cha kamisheni ya pamoja ya JCPOA kilichofanyika mjini Vienna, Austria hapo jana.

Amesema: Anga ya shaka, hatihati na mkanganyo iliyojengwa na serikali mpya ya Marekani kuhusu mustakabali wa JCPOA haiendani na matini na madhumuni ya makubaliano hayo; na Iran italifuatilia suala hilo muhimu.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran anayehusika na masuala ya sheria na kimataifa amefafanua kuwa makubaliano ya nyuklia yanaitaka Iran ipunguze shughuli zake za nyuklia, na kwa upande mwengine yanazitaka pande zingine zifute vikwazo vyote dhidi ya Iran vinavyohusiana na masuala ya nyuklia; lakini licha ya hatua ya Iran ya kuheshimu makubaliano ya JCOPA kuthibitishwa na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA), kungali kuna matatizo makubwa katika uondoaji athirifu na wa pande zote wa vikwazo dhidi ya Iran.

Abbas Araqchi

Araqchi amesisitiza kuwa Iran inataraji kuwa nchi zinazounda kundi la 5+1 zitaufikishia ulimwengu ujumbe mzito na wa pamoja kwamba pande zote husika zina wajibu wa kuheshimu na kutekeleza ahadi zao kuhusiana na JCPOA.

Kikao cha saba cha kamisheni ya pamoja ya JCPOA kilifanyika jana mjini Vienna kwa kuhudhuriwa na ujumbe wa Iran, nchi tano za kundi la 5+1 na mwakilishi mwandamizi wa Umoja wa Ulaya.

Tarehe 14 Julai 2015, Iran na nchi zinazounda kundi la 5+1 ambazo ni Uingereza, Ufaransa, Russia, China, Marekani na Ujerumani zilisaini mkataba kuhusiana na shughuli za nyuklia za Iran ambao utekelezaji wake ulianza Januari 16 mwaka uliopita wa 2016.

Hata hivyo Marekani, ambayo ni mmoja wa wanachama wa kundi la 5+1 inakwepa kutekeleza ahadi zake na badala yake imekuwa ikichukua hatua ambazo zinakiuka makubaliano hayo ya nyuklia.../

Tags