Iran yajadidisha uungaji mkono wake kwa Palestina katika ujumbe kwa Haniya
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amemtumia salamu za pongezi Ismail Haniya kwa kuteuliwa kuwa Mkuu mpya wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina Hamas.
Katika barua hiyo ya pongezi, Mohammad Javaz Zarif amekariri msimamo na uungaji mkono wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa Wapalestina na harakati zao za mapambano dhidi ya utawala ghasibu wa Israel.
Dakta Zarif amemkumbusha Haniya juu ya majukumu mazito ambayo yako mbele yake, katika kipindi hiki nyeti kwa Palestina na eneo la Mashariki ya Kati.
Kadhalika Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amemtaka Mkuu mpya wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina Hamas, kufuata nyayo za watangulizi wake, katika kusimama kidete na kuunga mkono muqawama mbele ya chokochoko za adui Mzayuni.
Amesisitiza kuwa, mapambano ndio njia pekee ya kushinda njama za Wazayuni na waitifaki wake, ambao wanafanya juu chini kuudhuru Uislamu, sanjari na kupanda mbegu za chuki na uhasama miongoni mwa Waislamu, ili kuwaweka katika mughafala wa kuishughulikia kadhia ya Palestina.
Mei 6, Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina Hamas ilimteua Ismail Abdulsalam Ahmed Haniya, mwenye umri wa 54, kuwa Mkuu mpya wa Ofisi ya Kisiasa ya harakati hiyo, kuchukua nafasi ya Khalid Mashaal.