Kiongozi Muadhamu: Maadui wanafanya njama ya kupotosha Mapinduzi ya Kiislamu
Kumbukumbu ya mwaka wa 28 tangu alipoaga dunia mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Imam Khomeini (MA) imefanyika leo kwenye haram ya kiongozi huyo kwa kuhutubiwa na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei ambapo maelfu ya watu kutoka maeneo tofauti ya Iran na wageni wa mataifa ya kigeni walihudhuria kumbukumbu hizo.
Katika kumbukumbu hizo, Kiongozi Muadhamu ameonya juu ya njama zenye lengo la kupotosha shakhsia ya Imamu Khomein i(MA) na mapinduzi ya Kiislamu na kuongeza kuwa, Imamu Ruhullah Khomein alifikia malengo ya harakati zake adhimu ambayo alikuwa akiyalingania kabla ya kufikiwa ushindi wa mapinduzi hayo. Kiongozi Muadhamu amesisitiza kuwa, shakhsia ya imamu na mapinduzi ya Kiislamu ya Iran ni mambo ambayo haviwezi kutengana na kwamba kumekuwepo na njama chafu za kupotosha shakhsia ya mwasisi huyo wa mapinduzi ya Kiislamu ya Iran.
Amesema kuwa, kabla ya mapinduzi ya Kiislamu, taifa la Iran lilikuwa likitawaliwa na utawala wa kidikteta tegemezi uliokuwa ukirithiwa ambapo utawala huo uliondolewa kwa kusimamishwa utawala wa kujitegemea wa wananchi. Ameongeza kuwa, mapinduzi hayo yalibainisha kwamba msimamo wa wananchi unaweza kuleta ushindi na mafanikio. Amefafanua kuwa, tangu siku ya kwanza ya ushindi wa mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran, maadui wa taifa hili wamekuwa wakitekeleza njama mbalimbali na kwamba hii leo Wairani wameweza kuvishinda vizingiti vya maadui hao. Amezungumzia utawala wa kifalme wa Aal-Saud nchini Saudia kwamba, katika safari ya Rais Donald Trump wa Marekani nchini humo, katika kujaribu kumridhisha rais huyo wa Marekani Riyadh ililazimika kutumia kiasi cha zaidi ya Dola bilioni mia moja kutoka katika hazina yake.
Aidha amezungumzia matatizo waliyonayo Waislamu wa nchi mbalimbali duniani zikiwemo, Syria, Yemen, Libya, Iraq na nyenginezo na kusisitiza kuwa, hii leo Waislamu wa Yemen wanapitia wakati mgumu sana ambapo wanafunga mwezi wa Ramadhani katika anga ya mashambulizi ya kila upande ya Saudia na washirika wake. Ayatullah Sayyid Ali Khamenei amesema: "Ninapenda kuwambia watawala wa Saudia kwamba, hata kama watashambulia Yemen kwa miaka mingine 10 au 20, kamwe hawatoweza kufikia malengo yao nchini humo."
Kuhusiana na maendeleo, Kiongozi Mudhamu amesema: "Kama tunahitaji kufikia maendeleo, tunahitaji kujiamini kwa yale tuliyoyapata katika mapinduzi ya Kiislamu." Katika sehemu nyingine, Kiongozi Muadhamu, amepongeza ushiriki mkubwa wa wananchi katika uchaguzi wa rais na mabaraza ya miji uliomalizika siku chache zilizopita, akisisitiza kuwa, uchaguzi huo ulitoa pigo kwa maadui wa taifa hili, kama ambavyo amesema kuwa, katika uchaguzi huo, mshindi wa kweli walikuwa ni wananchi wa Iran.
Hotuba kamili ya kiongozi Muadhamu katika kumbukumbu ya mwaka wa 28 tangu alipoaga dunia mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Imam Khomeini (MA) itakujieni katika matangazo yetu ya hapo kesho.