Iran yakadhibisha madai ya US kuwa inakandamiza uhuru wa kuabudu
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amepuuzilia mbali madai yaliyotolewa na Marekani kwamba hakuna uhuru wa kuabudu hapa nchini.
Bahram Qassemi amesema ripoti ya Marekani inayodai kuwa uhuru wa kuabudu umeminywa hapa nchini ni madai ya urongo, yasiyo na msingi na yanayoegemea upande mmoja.
Qassemi amesema ripoti hiyo imebuniwa kwa maslahi ya kisiasa ya Washington ambayo inajaribu kuficha rekodi yake nyeusi juu ya ubaguzi wa kidini, rangi, sambamba orodha ndefu ya kesi za maafisa usalama kuwashambulia wafuasi wa dini ya Kiislamu nchini humo.

Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni wa Iran ameongeza kuwa, uwepo wa dini na madhehebu tofauti haujawahi kuonekana kama tishio hapa nchini, bali umekuwa ukionekana kuwa fursa ya kipekee ya kuimarisha umoja wa kitaifa, mshikamano na maendeleo.
Hivi karibuni Rais Hassan Rouhani wa Iran alisema serikali inapania kutumia suala la dini na madhehebu tofauti hapa nchini kuelekea kwenye shina la umoja wa kitaifa na utamaduni.
Alisisitiza tangu huko nyuma Jamhuri ya Kiislamu imekuwa ikisisitizia suala la kuimarishwa umoja na mshikamano pasina na kuruhusu kugawanywa kwa misingi ya dini na madhehebu.