Rouhani: Mabadiliko yoyote ya mipaka yanahatarisha usalama na uthabiti M/Kati
Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitizia udharura wa kuimarishwa serikali kuu za Iraq na Syria na kufafanua kuwa, mabadiliko yoyote ya mipaka ya kijiografia wakati huu yatasababisha ukosefu wa usalama na uthabiti katika eneo lote la Mashariki ya Kati.
Rais Rouhani aliyasema hayo jana Jumatatu hapa mjini Tehran, alipokutana na kufanya mazungumzo na Mkuu wa Majeshi ya Uturuki Jenerali Hulusi Akar.
Dakta Rouhani amebainisha kuwa, kukabiliana na ugaidi na kulindwa mipaka ya kijiografia ya nchi za eneo ni mambo ya msingi ambayo Iran na Uturuki zinalenga kufikia kwa shabaha ya kuimarisha ushirikiano na uhusiano wa pande mbili.
Kwa upande wake, Mkuu wa Majeshi ya Uturuki Jenerali Hulusi Akar amesema Ankara inaheshimu uhuru wa kujitawala nchi zote za eneo hili na kwamba iko tayari kushirikiana na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika kukabili adui mmoja wa nchi mbili hizi, ambayo ni ugaidi.
Kabla ya mazungumzo na Rais Rouhani, Mkuu wa Majeshi ya Uturuki Jenerali Hulusi Akar ambaye aliwasili Tehran Jumapili usiku alikutana na kufanya mazungumzo na Mkuu wa Majeshi ya Iran Meja Jenerali Mohammad Baqeri na wawili hao wakabainisha uungaji mkono wao kwa umoja na kulindwa ardhi yote ya Iraq.
Septemba 25, Serikali ya Kieneo ya Kurdistan (KRG) ilipuuza mashinikizo ya serikali ya Iraq na jamii ya kimataifa ya kutoitisha kura ya maoni kwa ajili ya kujitenga eneo hilo.