Kamal Kharrazi: Mgogoro wa Lebanon unatokana na uchochezi wa Saudia
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i36316-kamal_kharrazi_mgogoro_wa_lebanon_unatokana_na_uchochezi_wa_saudia
Kamal Kharrazi, waziri wa zamani wa mambo ya nje wa Iran ambaye hivi sasa ni mkuu wa Baraza la Stratijia za Uhusiano wa Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, mgogoro wa hivi sasa wa kisiasa wa Lebanon unatokana na uchochezi wa wazi wa Saudi Arabia.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Nov 11, 2017 07:39 UTC
  • Kamal Kharrazi: Mgogoro wa Lebanon unatokana na uchochezi wa Saudia

Kamal Kharrazi, waziri wa zamani wa mambo ya nje wa Iran ambaye hivi sasa ni mkuu wa Baraza la Stratijia za Uhusiano wa Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, mgogoro wa hivi sasa wa kisiasa wa Lebanon unatokana na uchochezi wa wazi wa Saudi Arabia.

Kharrazi amesema hayo pambizoni mwa kikao cha Baraza la Ulaya mjini Vienna, Austria na huku akigusia athari mbaya za uchochezi wa Marekani na Saudia katika migogoro ya eneo la Mashariki ya Kati na Lebanon amesema kuwa, uchochezi wa siku za hivi karibuni wa Riyadh umekuwa na taathira mbaya za kiuchumi na kisiasa kwa Lebanon.

Saad Hariri, Waziri Mkuu wa Lebanon aliyetangaza kujiuzulu akiwa nchini Saudi Arabia. Lebanon imekataa kujiuzulu kwake na inasema, Saudia imemuweka katika kifungo cha nyumbani

 

Vile vile amesema, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imewanyooshea mkono wa urafiki majirani zake wote na anatumai kwamba nchi za eneo hili zitashirikiana katika kuimarisha usalama na utulivu wa eneo hili zima.

Waziri huyo wa zamani wa mambo ya nje wa Iran aidha amesema, Tehran iko tayari kuzidisha ushirikiano wake na nchi za Ulaya katika eneo la Mashariki ya Kati na iwapo nchi za Ulaya zinatilia maanani suala la kuwa na mustakbali mzuri katika eneo hili, basi hazina njia nyingine isipokuwa kukubaliana na hali halisi inayotawala hivi sasa kwenye eneo hili nyeti na muhimu mno.