Iran, Russia, Uturuki zakutana kujadili kadhia ya Syria
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i39235-iran_russia_uturuki_zakutana_kujadili_kadhia_ya_syria
Msaidizi wa ngazi za juu wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran katika masuala maalumu ya kisiasa, mwakilishi maalumu wa Rais wa Russia katika masuala ya Syria na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki wamekutana leo mjini Sochi, Russia kuzungumzia utatuzi wa mgogoro wa Syria.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 20, 2018 12:12 UTC
  • Iran, Russia, Uturuki zakutana kujadili kadhia ya Syria

Msaidizi wa ngazi za juu wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran katika masuala maalumu ya kisiasa, mwakilishi maalumu wa Rais wa Russia katika masuala ya Syria na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki wamekutana leo mjini Sochi, Russia kuzungumzia utatuzi wa mgogoro wa Syria.

Shirika la habari la IRNA limeripoti habari hiyo leo na kuongeza kuwa, Hossein Jaberi Asari, Msaidizi wa ngazi za juu wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran katika masuala maalumu ya kisiasa ameshiriki katika kikao hicho kilichowashirikisha pia Alexander Lavrentiev, mwakilishi maalumu wa Rais wa Russia katika masuala ya Syria na Sedat Onal, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki na pande hizo tatu zimejadiliana masuala yanayohusiana na kikao cha mazungumzo ya kitaifa ya Syria kinachotarajiwa kufanyika tarehe 29 na 30 mwezi huu wa Januari, mjini Sochi.

Wanajeshi wa Syria wakisherehekea ushindi

 

Mwanzoni mwa kikao hicho cha leo, mwakilishi maalumu wa Rais wa Russia katika suala la Syria ametoa ripoti fupi kuhusu mazungumzo hayo na baada ya hapo ujumbe wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na ule wa Uturuki, kila mmoja umetoa mtazamo wake.

Maafikiano kuhusu kuitishwa kongamano la mazungumzo ya kitaifa ya Syria mjini Sochi, yalifikiwa katika kikao cha wakuu wa Iran, Russia na Uturuki kilichofanyika mwezi Novemba mwaka jana mjini humo.

Hossein Jaberi Asari, Msaidizi wa ngazi za juu wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran katika masuala maalumu ya kisiasa na ambaye ndiye mkuu wa timu ya mazungumzo ya Iran katika mazungumzo ya Astana, jana Ijumaa aliekea nchini Russia akiongoza ujumbe wa ngazi za juu wa Iran kwa ajili ya kushiriki kwenye mazungumzo hayo.